Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuongeza majimbo pekee hakuimarishi demokrasia

Muktasari:

Kwa mujibu wa Nec, mgawanyo wa majimbo utazingatia idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano na hali ya kijiografia, ambavyo ni sehemu ya vigezo vingi vilivyotumiwa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inatarajiwa kutangaza majimbo mapya muda wowote, ikiwa ni kuboredha demokrasia kwa kuongeza uwakilishi wa wananchi kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Nec, mgawanyo wa majimbo utazingatia idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano na hali ya kijiografia, ambavyo ni sehemu ya vigezo vingi vilivyotumiwa.

Kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu, ni dhahiri kuwa Nec inatarajiwa kutangaza ongezeko la majimbo kutoka 232 ya sasa. Ukijumlisha na idadi ya wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi, viti maalumu, wateule wa Rais na Spika kama hatoki bungeni, jumla ya wabunge ni 323.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alisema kwa kawaida mgawanyo wa majimbo unatakiwa kufanyika kila mara, hasa kwa kila baada ya miaka kumi. Alisema mara ya mwisho ulifanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwamba wamelazimika kufanya mgawanyo mwaka huu kwa kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi.

Uchaguzi Mkuu utakaoiweka Serikali ya Awamu ya Tano umepangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, na kwa sasa kazi ya uandikishaji wapigakura inaendelea kote nchini, ingawa kwa kusuasua.

Kugawanya majimbo si jambo baya kwa kuangalia dhana nzima ya uwakilishi, lakini inapokuja suala la gharama za kuipanua demokrasia kwa njia hiyo kwa nchi changa kama Tanzania ndiyo shaka yetu inapokuja.

Hatuamini kwamba njia pekee ya kuimarisha demokrasia ni kuongeza uwakilishi wa wananchi kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, wakati kazi anazozifanya bungeni zimetajwa kikatiba kuwa ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

Wabunge wamejaribu kuifanya vizuri kazi yao ya kuisimamia na kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali kama ukusanyaji kodi, udhibiti wa fedha za umma, udhibiti wa ufisadi, uimarishaji wa huduma kwa wananchi, mbinu za kuongeza ajira, kuboresha kilimo, kuinua viwanda na hata kuimarisha demokrasia, lakini ushauri huo umekuwa haufanyiwi kazi.

Badala yake, wabunge wanaotoka upande unaoongoza Serikali wamegeuza chombo hicho kuwa uwanja wa siasa wa kuwashambulia wenzao, ambao wanajaribu kutekeleza majukumu yao ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

Na pengine ndiyo maana mambo hayaendi kama inavyotakiwa. Badala yake, uwezo wa Serikali kukusanya kodi umekuwa mdogo kiasi kwamba inashindwa kutekeleza bajeti yake kama Bunge linavyoidhinisha, kashfa za ufisadi zinaendelea, huduma kwa jamii zinazidi kuzorota, ajira kwa vijana inazidi kuwa ndoto, kilimo kinaendelea kuporomoka, viwanda vinazidi kuanguka huku demokrasia ikizidi kuminywa.

Kwa hiyo, yote hayo na mengine mengi hayatokani na uwakilishi wa wananchi kutokuwa mzuri, bali mfumo wa kuiwajibisha Serikali bado haujawa mzuri na hivyo uwajibikaji unazidi kuwa mdogo na utendaji wa ufanisi unazidi kupungua.

Wananchi hawahitaji kuwa na wabunge wengi kwenye eneo moja, bali wanataka kuona mfumo wa uongozi unakuwa na ufanisi kuanzia ngazi ya uongozi wa serikali za mitaa. Hawataki kuona Serikali ikipuuza ushauri wa Bunge na kutofuata maelekezo ya Bunge.

Tunaamini wananchi wakiona Bunge linafanya kazi yake kwa ufanisi, ndipo watakapoona haja ya kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Kwa mantiki hiyo, Nec haikutakiwa kutekeleza moja ya majukumu yake ya kuongeza majimbo bila ya kuangalia umuhimu wake kwa wakati huu, hasa hali ya kifedha ya Serikali. Kuongeza idadi ya wabunge kwa sasa ni kuwabebesha wananchi mzigo mkubwa zaidi na kuipunguzia Serikali uwezo wake wa kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyodhihirika kwenye bajeti za wizara nyingi mwaka huu.