Mbunge ataka kupiga sarakasi bungeni
Muktasari:
- Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatey Massay amemuomba Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amruhusu apige sarakasi bungeni, ili Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na naibu wake wajue amekasirika kwa kutojengwa kwa barabara ya Karatu Mbulu, Haidom hadi Sibiti.
Dodoma. Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM) Flatey Massay amemuomba Naibu Spika Dk Tulia Ackson amruhusu apige sarakasi bungeni, ili Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na naibu wake wajue amekasirika kwa kutojengwa barabara ya Karatu Mbulu, Haidom hadi Sibiti.
Masay amesema hayo leo Mei 17 2021 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2021/2022.
Amesema iwapo rasilimali za nchini zinagawanywa kote, basi zigawanywe kwa usawa na si wabunge wengine kutengewa bajeti na wengine kuachwa.
Massay amesema barabara hiyo imetolewa ahadi na marais wote waliopita, lakini ujenzi wake haujaanza na kwenye bajeti hiyo pia haijatengewa fedha za ujenzi licha ya umuhimu wake.
“Wananchi wametuma mwakilishi wao na tumeeleza leo naangalia kitabu cha bajeti mheshimiwa kwangu hakuna barabara, wengine wamewekewa bajeti ya ukarabati barabara lakini sisi hatujawahi kuona barabara ya lami kabisa,”amesema.
Amehoji ni lini changamoto hiyo itaisha na kwamba akipata nafasi ya kushika shilingi atashika hadi mwisho, ili kuhakisha barabara hiyo inajengwa.
“Mimi mtaalamu wa sarakasi niruhusu, nipande hapa nipige sarakasi tatu nne, ili mheshimiwa waziri na naibu wake ajue mbunge amechukia,”amesema.
Amemuomba Dk Tulia amruhusu, ili wajue kuwa ametumwa na wananchi wa jimbo la Mbulu Mjini kuomba barabara.
Hata hivyo, Dk Tulia alimtaka kutopiga sarakasi kwa sababu anamlinda na asiumie katika viti vya Bunge.
Akiendelea kuchangia Masay amesema hali imeshakuwa mbaya wananchi wanataka barabara, lakini waziri haelewi.
“Asiposema anajenga lini (wakati anahitimisha) lasivyo hatuelewani kama sarakasi nitapiga zote haiwezekani wengine wapate sisi tusipate,”amesema.