Mbunge ataka tembo wapatiwe uzazi wa mpango

Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate akizungumza leo Jumatatu Juni 5,2023 wakati akichangia kwenye hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2023/24 bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate ameomba Serikali kuwapatia tembo uzazi wa mpango ili kupunguza kasi ya kuzaliana.

Dodoma. Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate ameomba Serikali kuwapatia tembo uzazi wa mpango ili kupunguza kasi ya kuzaliana.

 Bilakwate ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 5,2023 wakati akichangia kwenye hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2023/24.

Mbunge huyo amesema hakuna namna nyingine kama Serikali inashindwa kuwavuna tembo ambao wamekuwa ni hatari kwa maisha ya wanadamu.

Mjadala wa Maliasili na Utalii kwa kiasi kikubwa umetawaliwa na kilio cha wabunge kuhusu kero ya tembo kwenye masuala ya mazao ambayo sasa wanatajwa kusababisha njaa na vifo.

“Katika eneo letu kwenye msitu waliletwa tembo kama 20 lakini sasa wameongezeka na kufikia 100, hivi kama hatuwezi kuwavuna basi wapewe uzazi wa mpango ili kupunguza kasi ya kuzaliana,” amesema Bilakwate.

Mbunge huyo amesema katika jimbo lake wanyama hao wamekuwa ni maadui wanaoharibu migomba na nyumba za watu lakini inasahangaza pale ambao serikali inataja kulipa fidia na kifuta machozi kwa nyumba iliyojengwa kwa gharama ya Sh20 milioni mwananchi analipwa Sh1 milioni.


Katika hatua nyingine Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela amesema kuwa tembo wanaingia kwenye majumba ya watu na kula wali uliopikwa yeye akitaja sababu kuwa huenda kwenye hifadhi wanakimbia kutokana na kukosa maji.

Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete yeye amesema kama hakutakuwa na uvunaji wa tembo, utafika wakati ambao Taifa litabaki na tembo lakini wananchi watakuwa wamekwisha wote kwa sababu wanyama hao siyo rafiki kwa maisha ya watu.