Mbunge atoa angalizo kodi biashara mtandaoni
Muktasari:
- Mbunge wa Viti maalum (CCM) Neema Lugangira ameitadharisha Serikali kwa uamuzi wake wa kuanza kutoza kodi kwa biashara na wahamasishaji (influencers).
Dodoma. Mbunge wa Vitimaalum (CCM), Neema Lugangira ametoa angalizo kwa Serikali wa uamuzi wake wa kuwatoza kodi wahamasishaji (influencers) biashara za mtandaoni kwa sababu kuna baadhi wanafanya hivyo kwasababu ya mahusiano na wenye biashara hizo.
Ameyasema hayo leo Juni 23, 2023 wakati akichangia hali ya uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti Kuu ya mwaka 2023/24.
Amepongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuanza kutoza kodi kwa biashara za mtandaoni lakini alitoa angalizo kwa kuwatoza influencers.
“Nataka kujua utambuzi wake kwasababu mtu anaweza kuwa nishabiki wa mtu fulani lakini akapost kazi zinazomhusu lakini hapati fedha ila amefanya kwa utashi wake na kwa namna ambavyo anamkubali,” amesema.
Amesema viongozi na wizara nyingi zimelipia katika kampuni ya Twiter ili wapate uthibitisho (verification) ambapo wanalipa gharama kwa Dola za Marekani 8 hadi 10 kwa mwezi.
“Napenda kufahamu pia wizara inampango gani wa kupata mapato kupitia fedha inayolipwa Twitter kupitia viongozi wetu wa Serikali na wizara husika?” amehoji.
Aidha, amehoji wanapanga kufanya nini ili kuhakikisha kwamba wanawake, vijana na makundi maalum wananufaika na asilimia 30 ya manunuzi ya umma kama jinsi sheria ya manunuzi ya umama imeelekeza.