Mbunge Chadema aliyepata ajali huyu hapa

Muktasari:

 

  • Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Zainab Mussa na dereva na abiri wengine, wamepata ajali ya gari eneo la Dumila mkoani Morogoro na anatarajiwa kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi zaidi.

Dar es Salaam. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Zainab Mussa amepata ajali ya gari eneo la Dumila mkoani Morogoro wakati akitoka jijini Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Zanzibar, Salum Mwalimu akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Februari 10, 2019 amesema mbunge huyo alikuwa njiani kurudi nyumbani kwake Pemba visiwani Zanzibar.

Pia, amesema mbunge huyo alipaswa kuhudhuria kikao cha kamati kuu ya chama hicho kinachofanyika leo Jumapili.

“Ni kweli amepata ajali, japo hatujapata taarifa za kitabibu zaidi ila ameumia katika eneo la kifua na alipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Dumila baadaye akapelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro na sasa wapo katika utaratibu ili wawalete Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),” amesema Mwalimu.

Mbali na mbunge huyo, abiria wengine waliokuwamo katika gari hiyo pamoja na dereva wamepatiwa huduma ya kwanza na watapelekwa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.