Mbunge CUF adai korosho itaipoteza CCM mikoa ya Kusini

Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali akilalamika bungeni wakati Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba alipokuwa akitetea hoja kufuta mgawo wa fedha zinazotokana na ushuru wa korosho zinazosafirisha nje zilizokuwa zikitolewa kwa wakulima, wakati akichangia mjdala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Ataka Serikali kutoa asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo

Dodoma. Sakata la kutaka Serikali kutoa asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi limeendelea kutikisa Bunge baada ya mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali kusema iwapo Serikali haitatoa fedha hizo utakuwa mwanzo wa kufa kwa chama tawala katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Waziri Mpango (Dk Philip-Waziri wa Fedha na Mipango) wewe ni mchumi. Watu wa Lindi na Mtwara tulikuwa maskini na zao la korosho ndilo lilikuwa mkombozi wetu, hatutakubali kukaa bungeni kama zao la korosho linakufa, tunakwenda kuandamana, mnaleta mabadiliko ya sheria, kwa kweli hili hatutakubali,” amesema Bobali.

 

Tayari baadhi ya wabunge wametishia kufanya maandamano iwapo Serikali haitatoa asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo.

 

Pia, wamepinga mabadiliko ya sheria ya korosho yanayokusudiwa kufanywa na Serikali ili ushuru huo upelekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

 

Bobali ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 22, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Serikali bungeni mjini Dodoma.

 

“Kuna Sh200 bilioni zinazodaiwa na wakulima, Waziri Mpango (Philip-Waziri wa Fedha na Uchumi) peleka hizi fedha wakulima wa korosho hatutakubali na habari hii si ndogo, hili jambo ni zito nawambieni CCM inakwenda kufa,” amesema.

 

Bobali aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Tuza Malapo aliyesema kuwa haiwezekani kuzungumzia uchumi wa mikoa ya Kusini bila kuzungumzia zao la korosho na kusisitiza Sh200 bilioni ni lazima zipelekwe  kwa wakulima.

 

“Mimi nimezaliwa Mtwara, nimesoma Mtwara kwa hiyo najua hili suala la korosho naomba kupata majibu ya hizi fedha. Waziri Mpango semeni hizi fedha mnazipeleka lini na ziko wapi. Tumekuita katika kikao mara kadhaa hukuja, na hii sheria mliyoileta najua itapita maana kila jambo likija humu ndani linapita,” amesema.