Mbunge Hanje aibua suala la Mwenge, Naibu Spika amjibu

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje ameibua sakata la mbio za mwenge akitaka kujua gharama zainazotumiwa na kama zitakuwa zinakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje ameibua sakata la mbio za mwenge akitaka kujua gharama zainazotumiwa na kama zitakuwa zinakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amemjibu kuhusu umuhimu wa mwenge huo, akisema una maanufaa makubwa kwani unakagua miradi ya maendeleo na yenye ubora wa chini inakataliwa na kwamba, wakimbiza mwenge wanamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Hanje ameibua hoja hiyo jana Jumatano April 6, 2022 wakati akichangia hotuba ya makadilio ya mapato na matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake ambapo ameomba mbio za mwenge zitazamwe upya.

Mbunge huyo amesema hana shida na umuhimu wa mbio za mwenge lakini shaka yake ni kiwango cha fedha kinachotumika kwa ajili ya ukimbizaji wa mwenge ambao gharama zake huwa haziwekwi hadharani katika matumizi yake ikiwemo kukaguliwa.

“Sina shida na suala la mwenge, natambua umuhimu wake kwa nchi yetu, lakini wakati mwingine tunatumia gharama kubwa na kuacha mambo ya msingi ikiwemo kushindwa kupeleka Sh1 bilioni katika mfuko wa vijana halafu hatujawahi kama Bunge kujadili fedha za mwenge na hazijawahi kukosekana,” amesema Hanje.

Mbunge huyo amesema kuna wakati mwingine mbio za mwenge zinaweza kutumia Sh900 bilioni lakini wakienda huko wanakagua miradi yenye thamani ya Sh400 au Sh1 bilioni jambo ambalo halina tija.

Ameshauri wasomi kutumia maarifa yao kubuni mbinu mbadala ya jinsi wanavyoweza kufanikisha ukimbizaji wa mwenge bila kutumia fedha nyingi kama ilivyo sasa.

Katika mchango wake, mbunge huyo amezungumzia ubunifu wa vijana unavyoshindwa kuendelezwa akilitaja gari la mchora katuni wa gzeti la Mwananchi, Masoud Kipanya kwamba huko ndiko Serikali ilitakiwa kujikita badala ya kuwaza vitu ambavyo havina tija.

Amesema kwa miaka minne sasa sera ya vijana ambayo inatoa dira lakini imeshindwa kutolewa huku akisisitiza suala la uwezeshaji wa kiuchumi kuhusu mfuko wa maendeleo ya vijana.

Mbunge huyo amekosoa mpango wa maendeleo wa vijana ambao unajikita katika makongamano, Semina, warsha na kujengeana uwezo badala yake amesema inatosha na hivyo ni wakati wa kujikita katika maeneo mengine.