Mbunge Kamani atilia shaka vijana, wanawake kupata mikopo asilimia 10

Muktasari:

  • Mbunge huyo ametaka Serikali izibe mianya ya ufujaji wa fedha ili kuweza kusaidia mpango wa maendeleo lakini akasisitiza ni muhimu kwa kusaidia kundi la vijana.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu Kundi la Vijana, Ng’wasi Kamani ametilia shaka fedha za mkopo wa vijana, wanawake na wenye ulemavu ambazo hutolewa na halmashauri kwamba huenda ziisitolewe katika mwaka wa fedha 2023/24.

Kamani ameonyesha hofu hiyo leo Jumanne Novemba 7, 2023 wakati akichangia bungeni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kujadili mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/25.

Mbunge huyo amesema katika mpango wa Serikali haoni kama kuna dalili za fedha hizo kutolewa kama ambavyo Serikali ilikuwa imeahidi na kwamba bila kufanya mageuzi makubwa itabaki kuwa ni kilio kwa kundi la vijana wa Tanzania.

Kingine mbunge huyo ametahadharisha wakati Serikali ikijiandaa kuanza kuutekeleza mpango huo, ni lazima itazame jinsi ya mivujo ya kwa kuwa kuna maeneo fedha zinatafutwa lakini kwingine zinaendelea kuliwa na watu wengine jambo alilosema ni baya na litakuwa mwiba kwenye mpango.

Ameitaka Serikali kuziba mianya hiyo ili iweze kusaidia katika mpango unaofuata ndipo kutakuwa na mafanikio makubwa kwenye mpango huo na ambao utakwenda kusaidia kundi la vijana kufikia ndoto yao.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, hata humu kwenye mpango, tunaona namna ambavyo kundi la vijana limesahaulika, Napata mashaka kama vijana watapa mkopo katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24 maana sioni dalili,” amesema Kamani.

Katika hatua nyingine Mbunge wa Chemba, Mohamed Moni amesema hakuna kitu chochote kinachofanyika kupitia magari yaliyonunuliwa ya Uviko 19 ambayo yalilenga kuchimba maji kwenye kila mkoa.

Moni amesema magari hayo uwezo wake ni mdogo lakini pia Serikali haitoi fedha za kuwalipa wakandarasi na kufanya mambo kuwa magumu kwenye huduma za maji hasa maeneo ya vijijini ikiwemo jimboni kwake ambako gari lina miezi 11 limesimama kijijini bila kuchimba maji na wananchi hawana maji.