Mbunge wa CCM, wadau washauri tatizo la vivuko Kigamboni

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

Hayo wameyaeleza leo Jumatano Aprili 24, 2024 katika mjadala wa X space ya Mwananchi uliokuwa na mada isemayo: Ipi suluhu ya kudumu ya changamoto ya huduma ya vivuko Kigamboni-Magogoni?





Dar es Salaam. Wananchi wa Wilaya Kigamboni jijini Dar es Salaam wamesema uchache wa vivuko katika kivuko cha Kigamboni unasababisha watu kushindwa kuvuka kwa wakati na kuwahi kwenye majukumu yao.

Hali hiyo hutokea kuanzia saa nne usiku kwa kuwa na kivuko kimoja na watu wanajikuta wanatumia muda mwingi kusubiria.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Aprili 24, 2024 katika mjadala wa X space ya Mwananchi uliokuwa na mada isemayo: Ipi suluhu ya kudumu ya changamoto ya huduma ya vivuko Kigamboni-Magogoni?

Miongoni mwa waliochangia katika mjadala huo,  ni Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile, ambaye amesema Kigamboni ina zaidi ya watu 300,000 na wanaotumia kivuko ni watu 50,000 hadi 70,000 na magari ni 2,000 kwa siku.

"Watu wengi wanafanya shughuli zao za kibiashara na makazini wanaishi Kigamboni kwa sababu wanakuwa jirani na Jiji la Dar es Salaam na kivuko kimekuwa njia kuu ya kuwasaidia kufika maeneo ya mjini," amesema Dk Ndugulile.

Kutokana na idadi ya watu aliyowataja ni wengi hivyo kumekuwa na changamoto ya kuhudumiwa na kivuko ambacho kimekuwa kikiharibika mara kwa mara na kuondolewa kwa Kivuko kikubwa cha Mv Kigamboni kumechangia kwa kiasi kikubwa mzigo kuwa mkubwa kwa vivuko vilivyopo.

Amesema vivuko vilivypo kwa sasa ni viwili na vinafanya kazi saa 24 pasipo kupumzika na kufanyiwa matengenezo makubwa imekuwa changamoto kubwa.

Dk Ndugulile amesema wananchi wa Kigamboni wanataka usafiri wa uhakika wa kuwafikisha mjini ndani ya muda mfupi na usalama wa maisha yao kwa kuwa vivuko hivyo vinaingiza karibia Sh20 milioni kwa siku licha ya kuwa na gharama kubwa za uendeshaji.

“Vivuko vilivyopo vinakosa sifa ya wanazozihitaji kwanza uhakika pili kutumia muda mfupi na tatu usalama," amesema Dk Ndugulile.

Akitolea mfano hai wa usafiri wa kwenda Zanzibar amesema hakuna Mtanzania anayegombania usafiri kwa sababu sekta binafsi inafanya kazi na kuna ushindani kila mmoja anapambana kuboresha huduma

Amesema kama Serikali inataka kuendelea na mfumo huo ni muhimu ikaruhusu sekta binafsi kufanya shughuli hiyo kutoa wigo mpana kwa wananchi kuchagua.

Hivyo ametoa ushauri wake kama Mbunge wa eneo hilo kwa Serikali ni kuona haja kuwa na vivuko hivyo vikabidhiwe sekta binafsi kwa sababu sera ya kushirikisha sekta binafsi ipo.

Naye Mkurugenzi wa Songoro Marine Transport Limited, Major Songoro ametoa mtazamo wake kuwa vyombo vya majini usalama wake ni mkubwa hivyo kuharibika kwake kunatokana na kutokufuata taratibu ikiwemo kutokufuata masharti ya kufanya  matengenezo kwa wakati na matumizi kuzidi kiasi.

"Mahitaji ya Kigamboni watumiaji ni wengi na yamekuwa yakiongezeka ukiangalia vivuko vilivyopo na ukitoa cha Magogoni hakipo vilivyopo kwa ujumla wake havikidhi mahitaji," amesema Songoro.

Songoro amesema anafahamu jitihada za Serikali katika kuboresha huduma lakini nguvu hiyo inapaswa kuongezeka kwa kununua vyombo vingine na vikarabatiwe kwa wakati.

"Vyombo vinavyoenda Zanzibar wanazingatia matengenezo, unakuta wanavyombo hata vinne kingine kinapumzika kingine kinafanyiwa matengenezo ndiyo maana hawezi kusikia Azam Marine imesimama wakati inaenda Zanzibar," amesema.

Amesema suluhisho la kudumu kwa mtazamo wake ni kuendelea kuboresha vyombo vikae vizuri na vihudumiwe kwa wakati.

Mhadhiri wa Chuo cha Baharia Dar es Salaam (DMI), Mhandisi Mlay Deism amesema kwa uzoefu wake aliongelea kuhusu matengenezo na watendaji wa kivuko.

"Matengenezo yanapaswa kuwa na mfumo mzuri, chombo kikiharibika kitengenezwe kwa wakati husika, lakini taratibu za manunuzi ya vyombo vya Serikali yanatumia muda mrefu inatakiwa kuwe na uharaka ili kurejesha huduma kwa wakati," amesema Mlay.

Kuhusu watendaji amesema wanapaswa kupewa elimu ya utendaji kazi mara kwa mara, kuongeza ufanisi kwa sababu kuna baadhi utendaji wao hauridhishi.

Mwananchi na mdau wa usafiri, Kimaro Wily amesema changamoto kubwa inayosumbua miradi mingi ni viongozi kukosa uwajibikaji hasa Afrika huku akipendekeza labda mkono wa chuma ulipaswa kutumika ili mambo yaende.

"Kuna matatizo tunayapata kwakuwa tunayatengeneza wenyewe kwa mfano matatizo ya vivuko vya Magogoni si kwamba yameshindwa kutatulika au havitengenezeki ni matatizo ambayo mafundi wapo.

"Chanzo cha matatizo ni sisi wenyewe na si kwenye vivuko tu na maeneo mengine si semi ni uvivu lakini aina ya maisha tunayoishi tunaona sawa iwe kwenye maofisi," amesema.

Said Rashid mchangiaji amesema changamoto za vivuko liko miaka mingi sasa na wataalamu wabobevu wapo kwenye taasisi za umma huku akishangaa na kuhoji au wanapeana kazi kindugu au upendeleo.

"Tatizo la kivuko cha Magogoni Juni mwaka 2023 Temesa (Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania) waliitoa taarifa kivuko kinashida kadhaa lakini ni mwaka umepita hakuna matengenezo ya kudumu, matatizo ni yale yale,” amesema Rashid.

Amesema shida ya Tanzania hakuna hulka ya kufanyakazi kwa muendelezo. Tukio likitokea waandishi wa habari wakatolea maelezo itapita wiki ya kwanza hadi ya tatu hakuna muendelezo wowote lakini vyombo vya nje wamekuwa wakifanya muendelezo.


Imeandikwa na Devotha Kihwelo na Tuzo Mapunda