Mbunge wa Mbarali alipuka wasaidizi wa Rais wasiwe wavivu kufikiri

Mbunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo akizungumza bungeni leo Jumanne Novemba 7, 2023.

Muktasari:

  • Mbunge huyo ambaye ameingia bungeni kupitia uchaguzi mdogo amesema hatakuwa tayari kuona wananchi wa Mbarali wakionewa kwa kuhamishwa na tayari ameshaomba kukutana na Rais.

Dodoma. Mbunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo amewaomba wataalamu wanaopata nafasi ya kumshauri Rais wasiwe wavivu wa kufikiri.

Mbunge huyo pia amemuomba Waziri wa Mipango, Profesa Kitila Mkumbo kusoma taarifa za mpango wa mataifa mengine kama Zambia, Congo na Mexico ili ajifunze namna walivyosaidia wananchi wao kwenye maeneo kama Mbarali.

Ndingo ametoa kauli hiyo jana Jumatatu Novemba 6, 2023 ikiwa mara yake ya kwanza tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo Oktoba 19, 2023 kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Francis Mtega kilichotokea Julai Mosi mwaka huu.

Amesema kitendo cha kuamua kuwaondoa wananchi wa Mbarali ili kupisha uhifadhi hakikubariki na hatakuwa tayari kuona hayo yakifanyika.

“Mnapanga kitu gani, mnafiri kuwaondoa wananchi wa wilaya hiyo bila huruma, tatizo mnaopata nafasi ya kumshauri rais mnakuwa wavivu wa kufikiri, achane na hayo ili muweze kumsaidia mheshimiwa Rais,” amesema Ndingo.

Mbunge huyo amesema kutokana na kinachoendelea, ameamua kumuandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan ili akamuone na kumpelekea kilio cha wananchi ambao wameshindwa kusaidiwa na wataalamu na watu wanaomsaidia mkuu huyo wa nchi.

Kwa mujibu wa Ndingo, mwaka 2008 Serikali ilihamisha vijiji karibu ya 10 na kata mmoja ilihamishwa yote kwa ajili ya kutunza mazingira lakini matokeo yake mazingira yaliharibika zaidi.

Amesema kutokana na hofu ya wananchi, hivi sasa wilaya hiyo inaongoza kwa wananchi wake kuugua magonjwa ya kisukari na presha (shinikizo la damu) na akahoji wananchi wanaotaka kuhamishwa wanapelekwa wapi.

Katika kipindi cha muda mrefu kumekuwa na kelele nyingi kuhusu wananchi wa Mbarali kutakiwa kuhama maeneo hayo kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji kwa madai wanaishi eneo oevu.