Mchakato kumpata mrithi wa Mrema TLP waanza

Muktasari:

Augustine Mrema ambaye alifariki duania akiwa na miaka 77, amekuwa mwenyekiti wa chama hicho tangu alipojiunga nacho mwaka 1999 akitokea NCCR Mageuzi.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita wiki mbili tangu Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema afariki dunia, chama hicho kimeanza mchakato wa kujaza nafasi yake.

Tayari imetangaza Ijumaa, Septemba 9, 2022, kikao cha sekretarieti kitafanyika ili kumpata atakayekaimu nafasi hiyo wakati mkutano mkuu ukiandaliwa.

Mwenyekiti mpya atapatikana kwenye mkutano mkuu baada ya kupigiwa kura na wajumbe wengi wa mkutano huo. Tarehe ya mkutano huo itatangazwa baadaye baada ya sekretarieti kufanya maandalizi.

Mrema alifariki Jumapili, Agost 21, 2022, saa 12.15 asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam. Amekuwa mwenyekiti wa chama hicho tangu alipojiunga nacho mwaka 1999 akitokea NCCR Mageuzi.

Akizungumzia mchakato huo leo Jumatatu, Septemba 5, 2022, Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo amesema mwenyekiti mpya atapatikana kwenye mkutano mkuu lakini sasa ameitisha kikao cha sekretarieti kwa ajili ya kukaimisha nafasi hiyo.

Amesema watakaoweza kukaimu nafasi hiyo ni makamu mwenyekiti mmoja wapo kati ya wawili waliopo ambao ni Hamad Mkadam (Makamu Mwenyekiti – Zanzibar) na Dominata Rwechungura (Makamu Mwenyekiti – Tanzania Bara).

“Utaratibu ni kwamba tunategemea kuwa na kikao cha sekretarieti ambacho kitakaimisha, baina ya makamu wenyeviti wawili, atoke mmoja ambaye atakaimu jhiyo nafasi mpaka mchakato wa mkutano mkuu utakapokamilika basi tutachagua mwingine,” amesema.

Lyimo amesema sekretarieti ikifanya kikao chake itaanza kufanya maandalizi ya mkutano mkuu ambao amesema hautakiwi kuchukua muda mrefu, amesema wanatarajia ndani ya miezi miwili uwe umefanyika.

Kuhusu utaratibu wa kumpata kaimu mwenyekiti, Lyimo amesema kuna vigezo viwili ambavyo vitatumika ambavyo ni kumwachia nafasi kiongozi ambaye ni mwandamizi zaidi au ipigwe kura kuchagua mmoja wapo.

“Kuna vigezo viwili, tunaweza tukaangalia yule ambaye ni senior (mwandamizi) au kikao kikaamua achaguliwe katika wale, ipigwe kura,” amesema Lyimo wakati akizungumza na Mwananchi Digital.