Mchakato sheria ya wazo bunifu mbioni kuanza

Muktasari:
- Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mchakato wa kutunga sheria ya wazo bunifu upo mbioni kukamilika akisema hivi sasa wanasuburi baraka za Baraza la Mawaziri.
Dar es Salaam. Serikali ipo katika hatua ya mwisho ya kuandaa wazo la sera ya Startup ' biashara bunifu ' iliyosubiriwa ambayo itawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuidhinishwa.
Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 wakati wa kikao cha wadau kujadili mchakato wa sera hiyo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema baada ya kupitishwa watatoa rasimu itakayojadiliwa na kuchukua maoni ya wadau kabla ya kutunga sera.
"... Mkutano wa leo na wadau wa ndani na nje ya nchi ni muhimu kwa mchakato huo na unatoa msingi wa hatua zinazokuja na tuko tayari kuendelea," amesema Nape.
Katika maelezo yake, amesema Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyowekeza katika miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), hatua iliyochangia sekta ya ubunifu kuwa na watu wengi zaidi. Hata hivyo, kwa muda kidogo sekta hiyo, imekuwa haina mfumo mzuri wa kisheria wa kuratibu ubunifu wa Tehama.
"Matokeo yake tunao vijana wa Kitanzania wanaofanya ubunifu lakini wanalazimika kwenda nchi jirani kuusajili ili ufanye kazi. Ndiyo maana Serikali tumeamua kuratibu jambo hili ili kuwa na mfumo mzuri wa kisheria utakaowatambua na kulinda ubunifu wao.
"Hatua hii itavutia uwekezaji kama ilivyokuwa katika mataifa mengine, mfumo wa kisheria unaanza na sera inayozaaa sheria na kanuni ili kuwalinda wabunifu wa Tehama na wawekezaji. Nimekuja kuwasikiliza wadau na kuwaeleza mchakato ulipofikia na utaratibu unaofuatwa," amesema Nape.
Waziri Nape amesema kikao hicho, kimewaleta wadau bunifu wa ndani ya nchi na nje ya nchi ili kujadili suala hilo na kuweka msingi bora wa kusonga mbele, akisema wamekubaliana kwa pamoja kuendelea na mchakato huo kwa hatua inayofuata.
Akielezea michakato iliyotangulia Mkurugenzi wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), Mohamed Mashaka amesema vitalu vya ujenzi wa sera za kuanzia vitaainisha na kutathmini changamoto muhimu na maeneo ya kipaumbele ya sera hiyo na vitahusisha mijadala ya mashauriano ya wadau mbalimbali ya kikanda.
Mashaka ameendelea kusema kuwa, "mchakato huo pia utahusisha kikundi lengwa cha mada ili kushughulikia mapungufu yaliyopo, kubainisha miunganisho na taratibu za utekelezaji na mapitio ya kina ya fasihi ili kuelewa hali ya sasa, mbinu bora ya kimataifa na mifano iliyofanikiwa."
Mkurugenzi Mkuu wa TSA, Zahoro Muhaji amesema wamekutana wadau mbalimbali wakiwemo wa maendeleo kuangalia namna ya kushirikiana katika kutengeneza sera bora za Startup ili kuleta ufanisi katika sekta hiyo.
"Kama unavyojua Serikali imedhalimia kuweka mazingira bora na wezeshi kwa vijana wanaonza biashara bunifu 'Startup' ndio maana wamepanga kutengeneza sera kwa kushirikiana na wadau.Ndio maana leo Serikali na wadau wengine tumekutana kuzungumza namna ya kusonga mbele.
"Tumekubaliana kuweka ratiba ya namna ya kulifanikisha jambo hilo na watakaoshirikisha kutoa maoni ya kuliboresha. Mheshimiwa Nape ametuambia kutakuwa na mfumo maalumu wa kutoa maoni kwa mtandao ili kutengeneza sera hii," amesema Muhaji.
Mdau wa sekta bunifu, Jumanne Mtambalike amesema sera ya Startup ikikamilika itatua na kutengeneza fursa mbalimbali kwa kampuni ndogo za Kitanzania. Amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio ikiwemo wadau kupata mrejesho kutoka Serikalini kuhusu suala hilo lilipofikia.
"Kwa vijana wabunifu wa teknolojia na wajasiriamali watarajie kufanikiwa kwa sera hii kutawasaidia kupata mitaji ya ndani na nje ya nchi na msaada kifedha ili kukuza biashara zao sambamba na kuwavutia wadau kutoka nje ya Tanzania," amesema Mtambalike.