Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mhariri Mwananchi ashauri Serikali iweke mjadala wa wazi kujadili sakata la VPN

Muktasari:

  • Akichokoza mada katika mjadala wa X-Space, wenye mada isemayo, Kuna tija kwa Serikali kusimamia matumizi ya VPN, Mhariri wa Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephraim Bahemu amesema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapaswa iweke mjadala kuangazia upya suala la katazo la huduma hiyo bila kibali ili kuweza kupata maoni ya wadau.

Dar es Salaam.  Mhariri wa Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephraim Bahemu amesema huduma ya matumizi binafsi ya mtandao wa intaneti (VPN) inaathari nyingi chanya kuliko hasi ikiwemo kuongeza ulinzi wa taarifa za mtumiaji pamoja na usalama wa mtandao hivyo mamlaka husika inapaswa itazame upya katazo lake.

Amesema kinachotakiwa mamlaka husika inapaswa iweke mjadala mkubwa watu watoe maoni waangalie athari na faida zake kisha kama nchi ichukue maoni yatakaoyokuwa na faida kwa taifa.

Bahemu ameyasema hayo leo Jumatano, Oktoba 18, 2023 wakati akichokoza mada kwenye mjadala wa X-Space unaoendesha na Kampuni ya Mwananchi Comunications Limited (MCL) wenye mada isemayo ‘Kuna tija kwa Serikali kusimamia matumizi ya VPN.’  

Amesema msingi wa VPN ni mfumo unaowezesha watu kutumia huduma za kidijitali kwa namna ambayo inalinda faragha. VPN inaweza kuficha taarifa za anayetumia mtandao huo na wengi wamekuwa wakitumia VPN kuzifikia huduma ambazo hawataki taarifa zao kuchukuliwa na wanaotoa huduma hizo.

“VPN pia inasaidia kuongeza nguvu ya mtandao, kurahisisha upatikanaji wa huduma za mtandao ambazo zimezuiliwa kwenye nchi husika,” amesema Bahemu

Kadhalika, amesema huduma hiyo inaweza kutazamwa kwa mtazamo hasi lakini kuna matumizi mengi chanya kuliko athari zake. Hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Serikali ingeruhusu mjadala wa jambo hili ili kufikia muafaka.

Amesema katika kulinda jamii dhidi ya maudhui yasiyofaa ni vyema wangewekeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa jamii wakiacha huduma za mtandao zikiendelea kukua kuliko kuzuia watu kuzifikia huduma za mtandao.

Ikumbukwe Oktoba 13, 2023, TCRA ilisema ni kosa kwa anayetumia VPN bila kibali faini yake ni Sh5 milioni au kifungo jela kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja suala ambalo limezua mjadala nchini.

Tayari baadhi ya wadau wanajipanga kufungua kesi mahakamani kupinga utekelezaji wa kanuni 16(2) ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ya maudhui mtandaoni ya mwaka 2020, inayokataza mtu kumiliki, kusambaza teknolojia, programu, kitu chochote kinachoendana au kuwezesha kupata maudhui yaliyokatazwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum Maxence Melo alinukuliwa na Gazeti la Mwananchi akisema: “tutakwenda mahakamani kupinga maamuzi hayo ya VPN na tutapinga matumizi ya kanuni hizo za 2020 kwa ujumla.”

Melo alisema Serikali inapaswa kuangalia upya uamuzi wa kudhibiti matumizi ya VPN. Alipendekeza Serikali ishirikiane na wadau wa masuala ya teknolojia na wafanyabiashara kushughulikia tatizo kwa kuzingatia haki ya kidigitali.

Pia, aliitaka Serikali kuheshimu na kulinda haki za Watanzania kupata habari, kupashana habari na kuwa huru mtandaoni.  

“Tupo tayari kushirikiana na wadau wengine kutafuta suluhisho kwa manufaa ya usalama wa taifa na kulinda haki za kidijitali,” alisema.

Leo Jumatano, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameweka wazi kuwa suala hilo ni njia ya Serikali kuufanya mtandao kuwa sehemu salama kutokana na matapeli.

Amesema mtandao ni sehemu ya kulindwa ukilinganisha na ukuaji wa teknolojia uliopo sasa pamoja na idadi ya watumiaji kuongezeka kila uchwao ambao kwa sasa wamefikia milioni 34, hivyo Serikali haina budi kuhakikisha usalama kwa kudhibiti waharifu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kongamano la saba la taifa la Tehama linalofanyika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Nape amesema kwa sasa utapeli unaendelea hivyo Serikali haina budi kuwatambua wale wote wanaotumia VPN.

Amesema zaidi ya nusu ya Watanzania wanatumia intaneti kwa sasa hivyo hata utapeli unaendelea ndio maana na Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kutunga sheria.

"Serikali imetunga sheria za kuwalinda watu wakiwa mtandaoni kama sheria ya (Data Protection), Miamala ya Kelektroniki, ni hatua moja wapo zilizokwisha chukuliwa," amesema Nape.

Amesema jambo la pili ni kutengeneza vyombo na mifumo itakayosaidia ulinzi huo ikiwemo Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Waziri Nape amesema kilichopo sasa waharifu wanabuni njia mbalimbali ndio maana, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imechukua hatua hiyo ya kutaka watu wajisajili wajulikane kwasababu kuna watu wanatumia mwanya huo kutekeleza uharifu kwa kujificha.