Prime
Kanuni zinazozuia VNP kupigwa kortini
Muktasari:
- Siku chache baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa katazo la matumizi ya mtandao binafsi (VPN) bila kibali, wadau wa mawasiliano wamesema wanajipanga kufungua kesi mahakamani.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa katazo la matumizi ya mtandao binafsi (VPN) bila kibali, wadau wa mawasiliano wamesema wanajipanga kufungua kesi mahakamani.
Kesi hiyo ni ya kupinga utekelezaji wa kanuni 16(2) ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ya maudhui mtandaoni ya mwaka 2020, inayokataza mtu kumiliki, kusambaza teknolojia, programu, kitu chochote kinachoendana au kuwezesha kupata maudhui yaliyokatazwa.
VPN ni mfumo wa teknolojia inayowezesha kuunda mtandao salama na wa faragha kwa kutumia mtandao wa umma kama vile intaneti.
Teknolojia hiyo hutumika kuchakata mawasiliano kati ya kifaa chako na kama kompyuta au simu na seva yake huficha na anuani yako (IP) na husaidia upatikanaji wa tovuti zilizozuiliwa.
Kutokana na hayo, TCRA kupitia taarifa kwa umma ilieleza imebaini upatikanaji wa maudhui yaliyokatazwa kupitia VPN, hivyo kumtaka kila anayetaka kutumia akajisajili kwenye mamlaka hiyo akiwa na anuani yake ya IP (utambulisho wa kifaa chake).
Hali hiyo itaiwezesha mamlaka hiyo kufikia kile ambacho mhusika amekuwa akitafuta kwenye mtandao na mahali alipopata alichokipata.
Hatua hiyo ilipingwa na wadau wa mawasiliano na siasa wakidai kinachofanyika ni kuminya uhuru wa utoaji na upatikanaji wa habari kidigitali.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxence Melo alisema Serikali inapaswa kuangalia upya uamuzi wa kudhibiti matumizi ya VPN.
“Haki ya kwenda mahakamani kupinga matumizi ya kanuni hizo ni ya kila mtu na wapo wadau wanaotaka kuchukua hatua hiyo, ikiwa watafanya hivyo sitapingana nao.”
Juzi wadau wa mawasiliano ya dijitali, waliitaka Serikali ishirikiane na wadau wa masuala ya teknolojia na wafanyabiashara kushughulikia tatizo kwa kuzingatia haki ya kidigitali.
Pia waliitaka Serikali kuheshimu na kulinda haki za Watanzania kupata habari, kupashana habari na kuwa huru mtandaoni.
“Tupo tayari kushirikiana na wadau wengine kutafuta suluhisho kwa manufaa ya usalama wa taifa na kulinda haki za kidijitali,” lilisema tamko la wadau hao.
Nia ya kuiburuza Serikali mahakamani inaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kampasi ya Dar es Salaam, Dk Joseph Matumaini aliyesema yupo tayari kushirikiana na watakaochukua hatua hiyo.
Alisema kisheria TCRA haikupaswa kutoa tamko la kuwataka wadau kujisajili ili kutumia VPN kabla ya kuitisha kikao cha kuwasikiliza.
“Katika ulimwengu wa mawasiliano huwezi kutoa tamko la namna hiyo bila kuwahusisha wadau kwa sababu haya ni masuala ya kisera, mambo ya sera mtu hawezi kuamka asubuhi na kutoa maelekezo hiyo haiwezekani. Pia kuna agenda ya imejificha kwa sababu tuna uhuru wa watu kuongea, unapoleta masharti kama hayo unamtesa,” alisema.
Dk Matumaini alisema kwa nchi yenye demokrasia na uhuru wa habari mfumo huo haukubaliki hata kama Bunge limepitisha kanuni hizo.
Kuhusu uwezekano wa TCRA kuwabaini watumiaji wa VPN wasiokwenda kujisajili, Dk Matumaini alisema uwezekano huo upo kwa kuwa teknolojia inabadilika kila baada ya miezi 18.
Kwanini watu hutumia VPN
Dk Matumaini alisema VPN hutumika kulinda faragha na uhuru wa mtu au taasisi isiingiliwe.
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC, VPN huimarisha mawasiliano na kulinda taarifa za siri za biashara na kusaidia ushirikiano wa kikanda, hivyo kudhibiti matumizi yake ni kuzuia ukuaji wa uchumi kupitia digitali.
Pia, VPN humlinda mtumiaji dhidi ya mtoa huduma wa mtandao kuona historia yake na kutazama namna mtu anavyovinjari mtandaoni.
Vilevile, husaidia kulinda vifaa vyako, ikiwa ni pamoja na kompyuta ya mezani, kompyuta ya mkononi na simu dhidi ya kuchunguzwa.
Unapojiunga na intaneti kupitia VPN, utambulisho wa kifaa chako (IP) hufichwa na kazi zako zote za mtandaoni hakuna anayeziona. Hii husaidia kulinda faragha za mtu na hata mtoa huduma za mtandao hawezi kupata taarifa hizo.
Kuhusu usalama, VPN hutengeneza ukuta wa kutoruhusu wadukuzi au wahalifu wa mtandao kupata au kuchukua taarifa za mtu mtandaoni.
Mbali na hayo, VPN humuwezesha mtu kupata taarifa zaidi nje ya mipaka ya nchi yake pamoja na kuwezesha upatikanaji wa taarifa zilizozuiliwa.
Kwa wale wanaotumia wi-fi , taarifa zao zinaweza kuwa hatarini kama hawana programu ya VPN inayosaidia kuweka uzio wa mtu kutumia mwanya wa kujiunga na mfumo huo kudukua taarifa zako.
Adhabu ya TCRA
Kulingana na kanuni, TCRA ina mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa sheria ikiwemo kuzia maudhui yaliyokatazwa.
Tayari TCRA imeziagiza kampuni ambazo matumizi ya VPN hayazuiliki, kutoa taarifa ndani ya mamlaka hiyo kabla ya Oktoba 30, 2023 wakiwa na kiambatanisho cha anuani ya itifaki ya mtandao IP.
Baada ya muda huo, yeyote atakayebainika kutumia programu hiyo bila kujisajili atakuwa ametenda kosa la jinai na adhabu yake Sh5 milioni, kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja.