Prime
TCRA kikaangoni katazo la VPN, wadau wacharuka
Dar es Salaam. Katazo la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu matumizi ya mtandao binafsi (VPN) bila kibali maalumu, limewaibua wadau wa mawasiliano na siasa, wakisema hatua hiyo inalenga kubana upatikanaji na utoaji wa habari kidijitali.
Katazo hilo lilitolewa juzi na TCRA kupitia taarifa yake kwa umma, ikieleza kubaini upatikanaji wa maudhui yaliyokatazwa kupitia matumizi ya VPN (Virtual Private Network) kinyume cha kanuni 16(2).
VPN ni mfumo wa teknolojia inayowezesha kuunda mtandao salama na wa faragha kwa kutumia mtandao wa umma kama vile intaneti.
Hutumika kwa kuchakata mawasiliano kati ya kifaa chako (kama kompyuta au simu) na seva yake huficha data yako na anwani yako ya IP.
Kutokana na hilo, hulinda faragha yako na kukusaidia kupata tovuti zilizozuiliwa au kuzungumza kwa usalama wa umma.
Hata hivyo, akizungumza jana na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema bado Serikali inaendelea kuwabana wananchi kupata na kupokea habari.
“Tangazo hilo linatoa tafsiri kwamba Serikali bado inataka kuendelea kubana wananchi katika kupata na kupokea habari, mfano mzuri ni wakati wa uchaguzi mitandao yote ilizimwa na wananchi wakakosa fursa ya kupata habari,” alisema Wangwe.
Alisema matumizi ya VPN kwenye mataifa mengine si ya kupiga marufuku, japo kwa nchi zenye dalili za udikteta ndio mambo hayo hutokea kwa lengo la kuwachagulia wananchi aina ya habari ya kupata.
Wangwe alikiri kweli VPN inaweza kutumika kupata picha zenye ukinzani wa kimaadili, lakini anashauri zitumike njia nyingine za kudhibiti maudhui yasiyofaa kuliko kushughulikia matumizi ya VPN.
“Wote wanaozalisha maudhui yasiyofaa au kusambaza washughulikiwe kwa kuwa wanafahamika na mitandao yao ipo,” alisema Wangwe.
Kanuni, taarifa ya TCRA
Kwa mujibu wa kanuni ya 16(2) ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya maudhui mtandaoni ya mwaka 2020, “mtu hatotoa, kusambaza, kumiliki teknolojia, programu na kitu chochote kinachoendana au kuwezesha mtu kupata maudhui yaliyokatazwa.”
Ukiwa ni utekelezaji wa kanuni hiyo, TCRA imeziagiza kampuni ambazo matumizi ya VPN hayazuiliki, kutoa taarifa ndani ya mamlaka hiyo kabla ya Oktoba 30, 2023 wakiwa na kiambatanisho cha anuani ya itifaki ya mtandao (IP Adress).
Taarifa hiyo iliyotolewa juzi na Mkurugenzi Mkuu TCRA, Dk Jabir Bakari ilifafanua kuwa maelekezo ya mamlaka hiyo yamezingatia kanuni ya 16 (b) ya mawasiliano ya kielektroniki na posta kuhusu maudhui ya mtandaoni za mwaka 2020.
Kanuni hizo zinaipa TCRA mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa sheria, ikiwamo kuzuia maudhui yaliyokatazwa.
“TCRA inapenda kuukumbusha umma utoaji, umiliki au usambazaji wa teknolojia, programu, programu tumizi au kitu chochote kinachoendana au kusaidia mtumiaji kupata maudhui yaliyokatazwa ni kosa la jinai,” inasema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa TCRA, mtu atakayebainika kutumia programu yenye kuruhusu au kusaidia mtumiaji kupata maudhui yaliyokatazwa ni kosa la jinai na adhabu yake ni Sh5 milioni, kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja.
Jana, Mwananchi ilimtafuta Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kupitia ujumbe wa maandishi na kumuuliza kuhusu sababu ya katazo hilo la VPN, naye alihoji, “umeona statement ya Serikali au TCRA.”
Hata Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari alipoulizwa kwa simu kuhusu katazo hilo, alisisitiza watu wanaotumia VPN kujisajili.
“Hata kama unakosoa, unaandika, kuna shida gani? Kama unakosoa, unatumia VPN, tumesema jisajili hapa,” alisema.
Wanachosema wadau
Hata hivyo, katazo hilo limeendelea kupingwa zaidi, huku Chama cha ACT Wazalendo kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma na Naibu Waziri Kivuli wa Habari na Tehama, Philbert Macheyeki akisema Serikali imeacha jukumu lake la kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu usalama na ulinzi wa taarifa za kimtandao, inazuia VPN.
“Badala ya kushughulikia wizi wa taarifa, utapeli na ulaghai wa kimtandao, Serikali inakuja na tamko linalolenga kurudisha nyuma hatua na kurahisisha udukuzi wa taarifa. Hii haikubaliki na inapaswa kupingwa kwa nguvu zote,” alisema Macheyeki kupitia taarifa yake kwa umma.
Macheyeki aliitaka Serikali kusitisha kanuni hizo kandamizi na kuacha wananchi, taasisi na mashirika kuendelea kuvinjari haki ya faragha, kupata na kutoa habari kama ilivyotolewa na katiba ya nchi.
Macheyeki alitoa wito kwa wadau wote kushikamana ili kulinda uhuru wa kupata habari nchini kwa kupinga katazo hilo na kutaka kanuni zifanyiwe marekebisho.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mdau wa mawasiliano, Carol Ndosi akisema kazi ya TCRA sio kuzuia mtandao tu, bali ina jukumu la kutoa elimu na kulinda masilahi ya watumiaji.
“Kufuata njia nyepesi ya kudhibiti matumizi ya VPN bila usajili kwa mtindo huu haitotatua tatizo la maudhui,” aliandika kupitia mtandao wake wa X.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamiiforums, Maxence Melo alisema matumizi ya VPN katika tafiti na mambo mengine binafsi yanasaidia mtu kutoingiliwa kwenye mambo yake.
“Moja ya athari za katazo hili ni kikwazo cha watu kujumuika kwenye mitandao kama Clubhouse, VPN ilikuwa inawapa wananchi kujumuika kote duniani kwenye mjadala na kuchangia mawazo yao, sasa kuleta zuio hili si kutaathiri tu uhuru wa kupata na kutoa taarifa, bali kunyima watu fursa ya kufahamu tamaduni mbalimbali,” alisema Melo.
Alisema VPN inawasaidia watu kulinda faragha zao dhidi ya uhalifu mtandaoni na kuzuia udukuzi wa taarifa, hivyo katazo hilo linatengeneza mazingira ya taarifa za watu kutokuwa salama.
Kwa athari za kiuchumi, Melo alisema katika dunia ya kidijitali VPN ni kifaa muhimu kuimarisha mawasiliano na kulinda taarifa za siri za biashara na kusaidia ushirikiano wa kikanda, hivyo kudhibiti matumizi yake ni kuzuia ukuaji wa uchumi kupitia dijitali.
Pia, alisema kuanzia Februari mwaka huu mtandao wa Clubhouse haupatikani nchini endapo mtu hatotumia VPN, hivyo zuio hilo litawanyima fursa Watanzania kujiunga na mtandao huo.
“Tunaitaka Serikali iangalie upya maamuzi ya kizuizi cha matumizi ya VPN, badala yake washirikiane na asasi za kiraia, wafanya biashara kushughulikia tatizo, tukizingatia haki ya kidijitali, Serikali iheshimu na kulinda haki za Watanzania kupata habari, kupashana habari na kuwa huru mtandaoni,” alisema.
Alisema wapo tayari kushirikiana na wadau wengine kutafuta suluhisho kwa manufaa ya usalama wa Taifa na kulinda haki za kidijitali.