Mchengererwa atangaza kiama watumishi Tamisemi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tamisemi, Mohamed Mchengerwa

Muktasari:

  • Waziri Mchengerwa ametangaza kiama kwa watumishi wa Tamisemi ambapo watakaoenda kinyume na taratibu zao za kazi hasa kwenye matumizi mabaya fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mtwara. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema ofisi yake imepokea zaidi ya Sh6.5 trilioni ambazo zimepelekwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali huku akitangaza kiama kwa wale watakaowachezea fedha hizo.

Waziri Mchengerwa amesema hayo leo Septemba 15, 2023 wakati akitoa salamu za wizara yake mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Manispaa ya Mtwara.

“Katika eneo la elimu tumepokea zaidi ya Sh2 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu nchi nzima na kugharamia elimu msingi bila malipo.

 “Kwenye Afya msingi tumepokea zaidi ya Sh1.5 trilioni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali za halmashauri, ukarabati wa hospitali kongwe, ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba, ujenzi wa zahanati pamoja na nyumba za watumishi,” amesema Mchengerwa.

Aidha kwenye eneo la miundombinu, Mchengerwa amesema kuwa zaidi ya Sh3 trilioni zimetumika kujenga, kuendeleza barabara za vijijini na mijini ambapo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2023, ujenzi wa daraja la Jangwani na uendelezaji wa bonde la Mto Msimbazi utatekelezwa.

 ‘Kwa fedha hizo ulizotoa, sisi wasaidizi wako hatuna sababu ya kutokufanya kazi, kujituma kwa bidii na weledi wa hali ya juu, sisi kazi yetu kubwa ni kupanga namna bora ya kusimamia na kutekeleza ufanisi wa kazi zilizokusudiwa kukamilishwa, kupitia fedha hizo," amesema Mchengerwa.

"Ninakumbuka siku chache zilizopita wakati unatuapisha, ulitusisitiza kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu kama ilivyo dira yako, nami nilipoanza kazi nilishusha wizara yako kwa wananchi na kuwataka  watendaji wote walio chini yangu kujishusha kwa wananchi na kutoka maofisini kwenda kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao."

“Yeyote miongoni mwetu atakayewachezea wananchi wako kwa uvivu, uzembe au ubadhirifu wa fedha unazozitoa (Rais Samia) kwa ajili ya huduma za wananchi, yule ambaye ni saizi yangu, nitashughulika naye kweli kweli.”

“Kwa kuwa umeniamini kuongoza wizara hii ninakuahidi kuisimamia kwa uadilifu mkubwa, kuendelea kuchapa kazi kwa bidii, kuongeza usimamizi kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha miradi yote iliyopata fedha inakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma bora na atakayefanya vinginevyo nitalala naye mbele," amesisitiza Mchengerwa.