Waziri Mchengerwa azungumzia maagizo ya Rais Samia uchaguzi 2024

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa.
Muktasari:
- Septemba 1, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan aliwaapisha viongozi mbalimbali aliokuwa amewateua hivi karibuni kisha alitumia hafla hiyo kumtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa kwenda kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema amejipanga kikamilifu kwenda kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwatumikia wananchi na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani.
Mchengerwa alikuwa miongoni mwa wateuliwa walioapishwa Jumamosi ya Septemba 1, 2023 kuwa Waziri wa Tamisemi, Ikulu ndogo Zanzibar. Awali, alikuwa waziri wa maliasili na utalii ambako nafasi yake imechukuliwa na Angellah Kairuki aliyekuwa Tamisemi.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema,“mwakani kuna kivumbi na mimi nakujua najua unaweza, kivumbi kile kinafanana na kifua chako najua unaweza, kwa hiyo nimekupeleka Tamisemi ni kazikazi ili mwakani tuseme vizuri.”
Kuhusu maagizo hayo, Mchengerwa akizungumza na Mwananchi Digital alisema,"mimi sina hofu nalo, kwani tafasiri ya Rais ni kwenda kufanya kazi, uchaguzi utakuwa mwepesi kama kila mmoja atafanya kazi usiku na mchana, Watanzania wanaona tumefanya nini.
Kama kuna sehemu hatutafanya kazi, basi utakuwa ni mgumu, lakini kama tutafanya kazi, tutatatua kero za wananchi, miradi itatekelezwa utakuwa uchaguzi mwepesi sana na kama hatutafanya haya basi utakuwa uchaguzi mgumu."
Aliongeza,"sisi tunakwenda kufanya kazi kwa bidii na maana yake tutakuwa tumetibu na kutatua kero za Watanzania na ndio tafasri ya Rais kama utakuwa umemwelewa ana maanisha nini. Hivyo tunakwenda kulifanya hili usiku na mchana kuwasogezea wananchi huduma."
Akisifu utendaji wa Mchengerwa katika hafla hiyo, Rais Samia alisema amemtaja kuwa mfano wa mabadiliko akitumia rejea ya alichokifanya kwa mara ya kwanza baada ya kumteuwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Tutakapowachambua hapa wengine ni mabingwa wa mabadiliko, nimseme hapa Mchengerwa (Mohammed) kwa mfano, nilipompeleka utumishi mwanzo ninamteuwa, kaingia na kasi kubwa kelele zikawa nyingi.
“Nikasema mmh… labda Waziri wangu kazidi kapandisha mabega, mpeleke michezo, kaenda michezo kazi aliyofanya mnaiona, kaacha kazi nzuri sana, katoka Michezo nimempeleka Utalii.
“Mipango aliyoiweka sekta ile nani anakwenda utalii Angellar, sekta ile ukienda kufuata yaliyowekwa sekta ile mambo yanakwenda kupanda, Hassan (Dk Abbas) yupo pale amefanya kazi nzuri sana wameweka mipango na Waziri kwako ni kusimamia utendaji, yatekelezwe yale yaliyowekwa,” amesema.