Mchengerwa awatangazia kiama MaDC, MaDED, kumshauri Rais awatengue

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema wakurugenzi wa halmashauri  na wakuu wa wilaya watakaoshindwa kukamilisha ujenzi  wa  madarasa ifikapo Desemba 31, mwaka huu watamshauri Rais kutengua nafasi zao.

Moshi. Wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji katika halmashauri nchini, ambao watashindwa kukamilisha ujenzi wa madarasa ifikapo Desemba 31, 2023  huwenda wakapoteza ajira  zao baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, kutishia ‘kuwasemea’ kwa Rais.

Mchengerwa ameyasema hayo Desemba 12, 2023 wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utendaji na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2022/23 katika jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Mchengerwa amesema haiwezekanai Serikali ipeleke mabilioni ya fedha katika maeneo yao halafu zitumike vibaya,  huku wanafunzi wakikaa katika majengo chakavu yanayoweza kuleta madhara.

"Kwa watendaji ambao watashindwa kutekeleza ujenzi wa madarasa na fedha walipewa mwaka mmoja uliopita au miezi kadhaa iliyopita, maana yake wajitathmini, ikifika Desemba 31 viti vyao tutawatafutia watu wengine na tutamshauri Rais.

"Kama ni mkurugenzi, tutampendekeza kwa Rais tutengue nafasi yake, kama ni Mkuu wa wilaya ameshindwa kusimamia tutapendekeza kwa Rais atengue uteuzi wake. Watanzania tunalipa kodi, fedha zinakuja kwenye halmshauri zetu na zinatumika vibaya, ubadhirifu, rushwa na uzembe, kama waziri ninayemsaidia Rais katika eneo hili, sitokubali,”amesema.

Aidha amesema hatarajii kuona kiongozi anayesubiri kupelekewa fedha za ununuzi wa madawati huku watoto wanakaa kwenye jengo lililochakaa na ambalo linaweza kuwaangukia wakati wowote. “Kama yupo asubiri nje ya mfumo, huku kiongozi mwingine akichua nafasi hiyo.

"Huu ni mwaka wangu wa 21 ndani ya utumishi wa umma, kwa sababu kuna wengine hawanifahamu vizuri, wanazungumza yale wanayoyajua, niwape salamu tu nimepita katika mifumo yote ya Serikali na  mihimili yote mitatu, kwenye Mahakama nimekaa miaka 13, katika Bunge nimekuwepo  na sasa ndani ya Serikali kwa miaka kama mitatu, maana yake najua kila kinachoendelea.

"Pale ambapo hatufanyi vizuri katika mkoa au wilaya ni kwa sababu watendaji wetu wameamua tusifanye vizuri, kwa kufikiria maisha yao bila kuwafikiria Watanzania,”amesema Mchengerwa.

Naye Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya menedeleo katika jimbo hilo.

Amesema  kwa kipindi cha bajeti ya mwaka 2022/23 Serikali imetoa Sh10.33 bilioni.