Mchimba madini anywa sumu akienda kuripoti Polisi

Muktasari:

  • Alikuwa akienda polisi kuitikia wito, yadaiwa kulikuwa na mgogoro na mke wake.

Arusha. Mchimbaji madini ya Tanzanite, Gamalieli Munisi, mkazi wa Muriet anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu ikidaiwa amefanya hivyo kutokana na kuchoshwa na migogoro ya ndoa ya muda mrefu kati yake na mkewe.

Munisi (48) maarufu Chinga anadaiwa kunywa sumu na baadaye kwenda Kituo cha Polisi Muriet ili akafie huko.

Inadaiwa amefikia hatua hiyo baada ya kuitwa kwenye dawati la jinsia kwa mahojiano juu ya shauri la mkewe aliloliwasilisha akidai kutishiwa kwa silaha.

Akithibitisha tukio hilo leo Machi 27, 2024, kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema mtu huyo aliyekuwa akienda kuripoti Kituo cha Polisi Muriet Machi 20, 2024 alionekana akitapika kuanzia geti la kuingilia na kisha kuanguka ndani ya viunga vya kituo hicho.

Amesema kwa usaidizi wa wasamaria wema aliwahishwa hospitali ya jirani ya Muriet kwa matibabu lakini alifariki kesho yake Machi 21 akiwa anapatiwa matibabu.

“Upelelezi wa awali unaoyesha mtuhumiwa amefariki dunia kwa kunywa sumu. Siku ya tukio Machi 20, 2024 asubuhi alikuwa anakuja kuripoti kituoni, lakini kabla ya kufika ndani ya chumba cha huduma watu walimuona getini akiingia huku anatapika na kisha kuanguka,” amesema Masejo na kuongeza:

“Baada ya kuanguka watu walijisogeza kumsaidia ndipo akasema amefanya hivyo kutokana na mgogoro na mke wake ambaye baada ya kupigiwa simu, alikiri kutumiwa sms (ujumbe mfupi wa maneno) na mumewe kuwa anakunywa sumu, ndipo ikabidi awahishwe hospitali chini ya uangalizi wa ndugu zake. Alifariki dunia kesho yake,” amesema Kamanda Masejo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mosses Andrew amesema siku ya tukio alimuona Munisi akiingia getini akiwa anayumba, huku akitapika, na alipofika karibu na jengo la kuingia ndani akaanguka.

“Nadhani hiyo sumu alikunywa huko alikotoka kwani alikuwa anakuja huku anayumba ndipo akaishiwa nguvu pale kwenye lile jiwe akaanguka. Tulipomfuata akasema apigiwe simu mke wake, akaonyesha namba kwenye simu yake akapigiwa,” amesema Mosses.

Amesema baada ya mke wake kupigiwa simu aliomba mumewe asaidiwe kwa kuwa alikuwa njiani akielekea polisi kwani alimtumia sms kuwa anakunywa sumu amkute Polisi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Field Force, Veronica Gutta amedai Munisi amefariki dunia kwa kunywa sumu kutokana na kushindwa kuhimili migogoro ya ndoa na mke wake.

“Hawa wanandoa hawajawahi kuja kwangu kuleta malalamiko yoyote, lakini nasikia walikuwa na mvutano hadi kwenda kushtakiwa Kituo cha Polisi Muriet. Siku ya tukio aliyokuywa sumu ni kwamba aliitwa na dawati la jinsia kwa ajili ya kusuluhishwa,” amesema.

Alipotafutwa mkewe kujua chanzo cha tukio hilo, simu yake iliita bila kupokelewa na baadaye ukatumwa ujumbe mfupi kuwa wako kwenye msiba Wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro kwa mazishi ya Munisi.