Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchiriku kuhamasisha kuhusu uhuru wa kujieleza

Muktasari:

  • Mradi wa Jenga Sauti utatumia muziki wa Mchiriku katika kuihamasisha jamii juu ya uhuru wa kujieleza kupitia wanawake wenye vipaji na kuurudisha kwenye chati muziki huo.

Dar es Salaam. Muziki wa Mchiriku utatumika kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu uhuru wa kujieleza.

 Akizungumza na wanahabari leo Desemba 12, 2023; Getrude Malizeni ambaye ni Meneja wa Sanaa katika mradi huo, amesema mbali na kurejesha muziki huo kwenye hadhi, pia utawapa fursa wanawake wenye vipaji kuihamasisha jamii.

Hiyo itakuwa sehemu ya mradi wa ‘Jenga Sauti’ uliozinduliwa na Taasisi ya Utetezi na Maendeleo ya Vyombo vya Habari Tanzania (Medea Tanzania).

“Mradi huu unatarajia kurudisha hadhi ya muziki wa mchiriku masikioni mwa mashabiki na kutumia nguvu ya muziki wa Kiswahili, kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uhuru wa kujieleza na ushirikishwaji wa kijinsia, kama haki za msingi za binadamu,” amesema Malizeni.

Kwa mujibu wa Malizeni, mradi huo utaambatana na shughuli mbalimbali zinazolenga kuwapatia kipaumbele wananchi kama chachu ya mabadiliko kupitia mfululizo wa matukio ya sanaa, majadiliano ya wazi pamoja na mafunzo kwa waandaaji wa muziki wa Mchiriku.

“Tunatambua kuwa muziki wa Mchiriku ulikuwa ukisikika na kutumika zaidi kama burudani hasa katika matukio muhimu ya kijamii na muziki huu umebeba dhima ya utamaduni wa Kiswahili kutokana na ala zinazotumika pamoja na asili yake,” amesema.

Akizungumzia mradi wa Jenga Sauti, Malizeni amesema unaangalia zaidi jinsi gani muziki huu unaweza kutambulika tena kama zamani na kutumika katika kuelezea mambo mbalimbali yanayoikumba jamii.

Katika hatua ya awali, amesema mradi huu umefanikiwa kushirikisha vikundi viwili vya muziki wa Mchiriku vya Jagwa Music na Atomic Advantage Music Band.

Vikundi hivyo vimeshapewa mafunzo yaliyojikita katika kuwajengea uwezo wahusika katika maeneo mbalimbali mawasiliano, urasimishaji wa kazi, masuala ya kifedha na usambazaji wa kazi kidijitali.

Mafunzo mengine ni pamoja na kufaya tathmini ya kazi zao na utunzi wa tungo zenye kuwasilisha ajenda ya ushirikishwaji wa kijinsia na haki ya uhuru wa kujieleza.

Mradi huu kwa sasa unatekelezwa Dar es Salaam kwenye Wilaya za Kinondoni na Temeke.