Mchuano mkali wa wavulana, wasichana matokeo kidato II 2020

Monday January 18 2021
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Mchuano mkali umeonekana kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kati ya wasichana na wavulana ambapo asilimia 91.61 ya waliofanya mtihani huo walifaulu kuendelea na kidato cha tatu wakati asilimia 8.39 wakishindwa kufurukuta.

Jumla ya wanafunzi 601,463 walifanya mtihani huo na kati yao 550,979 wamefaulu na wanafunzi 50,484 hawakufanya vizuri hivyo watalazimika kurudia kidato cha pili kwa mwaka mwingine.

Angalia hapa matokeo ya kidato cha pili 2020/2021

Takwimu zinaonyesha wasichana waliofaulu ni 295,977 sawa na asilimia 91.43 na wavulana ni 255,002 sawa na asilimia 91.82.

Angalia matokeo hapa

Katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa wasichana wameng’ara zaidi kwa kuingia saba na kushika nafasi tatu za juu huku kukiwa na wavulana watatu pekee kwenye orodha hiyo.

Advertisement

Nankondo Mnyone wa Feza Girls ndiye aliyengoza kwa ufaulu akifuatiwa na Tiffany Kazael, Faraja Ahmed na Eward Rugaimukamu wote wa Canossa.

Lukas Lutengano wa Shule ya Sekondari Kibasila ameingia kwenye orodha hiyo kwa kushika namba tano na akiwa mwanafunzi pekee kutoka shule za serikali kuingia kwenye 10 bora.

Mwanafunzi huyu pia ameongoza orodha ya wavulana 10 waliofanya vizuri zaidi kwenye mtihani huo. Sambamba na Lucas orodha hiyo ina wavulana wengine wawili kutoka sekondari ya Chang’ombe na waliosalia saba wanatoka shule binafsi.

Nafasi ya sita imeshikwa na Benjamin Mwakapalila wa Feza Boys akifuatiwa na Namara Lwansa na Nuran Majid wa Feza Girls wakati nafasi ya tisa imekwenda kwa Junior Mkeni wa Jude na orodha ya kumi bora ikihitimishwa na Hope-Rosemary Semsela wa Feza Girls.

Kulingana na Katibu Mtendaji wa Necta Dk Charles Msonde ufaulu huo umepanda kwa asilimia 1.57 ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo asilimia 90.04 ya waliofanya mtihani huo walifaulu.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi wamefanya vizuri zaidi katika masomo ya uraia, historia, Kiswahili, Kiingereza, baiolojia, biashara na uhasibu ambapo ufaulu wa masomo hayo upo juu ya wastani kati ya asilimia 50.70 na asilimia 92.38 na wengi wakianguka kwenye masomo ya jiografia, fizikia, kemia na hisabati.

Kwa mujibu wa matokeo hayo shule 10 bora ya kwanza ni St Francis Girls ikifuatiwa na Kemebos, Bright Future Girls, Canossa, Tengeru Boys, Centennial Christian, St Monica Moshono Girls, Marian Boys, Precious Blood na Feza Boys.

St Francis Girls, Kemebos, Canossa na Feza Boys zimeng’ara pia kwenye orodha ya shule kumi bora kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba hadi Desemba 2020.


Advertisement