Mvuto, mshangao matokeo kidato cha nne, kidato cha pili

Sunday January 17 2021
mvuto pic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Ni matokeo ya kushangaza na yenye mvuto wa aina yake. Ndivyo unavyoweza kuyaelezea matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2020 yaliyotangazwa juzi.

Wakati Shule ya St Francis ikiibuka kinara kwa kushika nafasi ya kwanza na kuiporomosha Kemebos hadi nafasi ya nne, orodha ya wanafunzi kumi bora imebebwa na wavulana saba huku watatu waliosalia wakiwa ni wasichana tena kutoka shule moja ya Canossa.

Katika matokeo ya mwaka 2020, Kemebos iliongoza katika orodha ya shule kumi bora ikifuatiwa na St Francis ambayo katika matokeo ya 2021, ni kama imelipiza kisasi kwa kushika nafasi ya kwanza, huku Kemebos ikishika nafasi ya nne.

Mshangao zaidi ni mwanafunzi wa kwanza kitaifa, Paul Luziga aliyetoka shule ya Panda Hill ya mkoani Mbeya, ambayo haipo katika orodha ya shule kumi bora. Kwa mujibu wa Necta shule hiyo imeshika nafasi ya 48 kitaifa.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema ufaulu umeongezeka hadi asilimia 85.84. Mwaka 2019 ufaulu ulikuwa asilimia 80.65.

Alisema kati ya waliofaulu, wasichana ni 193,672 sawa na asilimia 85.44 na wavulana ni 180,286 sawa na asilimia 86.65.

Advertisement


Ufaulu kimasomo

Kuhusu ufaulu wa kimasomo, Dk Msonde alisema takwimu zinaonyesha kwamba watahiniwa walifanya vizuri kwenye masomo mengi ya msingi na kwamba, ufaulu wa masomo hayo uko juu ya wastani ambao ni kati ya asilimia 50.53 na 94.83.

Alisema takwimu zinaonyesha watahiniwa hawakufanya vizuri katika masomo mawili ya fizikia na hisabati, japo katika somo la fizikia ufaulu umeendelea kuimarika kutoka asilimia 48.38 mwaka 2019 hadi asilimia 48.87 mwaka 2020.

Masomo yenye ufaulu wa juu ni Kiswahili (asilimia 94.83), kemia (asilimia 87.09), Kiingereza (asilimia 73.55), uhasibu (asilimia 65.84) uraia (asilimia 65.83) na jiografia (asilimia 53.90), huku somo la hisabati likiwa chini kwa ufaulu wa asilimia 20.12


Shule binafsi zatamba

Kama ilivyo katika miaka takriban 10 ya matokeo hayo, shule binafsi zimezidi kujihakikishia nafasi katika orodha ya shule kumi bora.Katika matokeo ya mwaka huu orodha hiyo imetawaliwa na shule binafsi ambazo ni St Francis Girls (Mbeya), Canossa (Dar) Kemebos (Kagera) Bethel Sabs Girls (Iringa) Feza Boys (Dar) na Ahmes (Pwani).

Shule nyingine ni St Aloyysius Girls (Pwani), Marian Boys (Pwani) na St. Augustine Tagaste ya Dar es Salaam.

Ilboru ndiyo shule pekee ya Serikali iliyoingia kwenye orodha ya shule 10 bora na ikifanikiwa kuingiza wavulana wawili kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora. Katika orodha hiyo ya wanafunzi 10 bora Mzumbe pia iliingiza wavulana wawili.


Wavulana watikisa

Matokeo hayo yanaonyesha kati ya wanafunzi 10 bora, saba ni wavulana huku watatu waliosalia wasichana wakitoka shule ya sekondari Canossa.

Wanafunzi hao ni Paul Luziga (Pandahill), Timothy Segu (Mzumbe), Isaya Rukamya (Feza Boys), Ashraf Ally (Ilboru), Samson Mwakabage (Jude), Derick Mushi (Ilboru) na Innocent Joseph (Mzumbe). Wasichana walioingia kumi bora ni Justina Gerald, Layla Atokwete na Lunargrace Celestine.


Shule 10 zilizoongeza ufaulu

Dk Msonde alizitaja shule 10 zilizoongeza ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo katika matokeo ya kidato cha nne.

Shule hizo ni Santakagwa (Rukwa), Mt Carmel (Kigoma), Trust Patrick (Arusha), Famgi (Mwanza), Kimali (Simiyu), St Rufino and Ronaldo Agr (Kigoma), Ilboru (Arusha), Rocks Hill (Mwanza), Songea Boys (Ruvuma) na Msalato (Dodoma).


Mchuano kidato cha pili

Akitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili, Dk Msonde alisema jumla ya wanafunzi 601,463 walifanya mtihani huo na kati yao 550,979 wamefaulu.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na mchuano wa ufaulu kati ya wasichana na wavulana baada ya kupishana kwa alama chache za ufaulu wa jumla. Wasichana waliofaulu ni 295,977 sawa na asilimia 91.43, huku wavulana waliokuwa 255,002 wakipata ufaulu wa asilimia 91.82.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi wamefanya vizuri zaidi katika masomo ya uraia, historia, Kiswahili, Kiingereza, biolojia, biashara na uhasibu ambapo ufaulu wa masomo hayo upo juu ya wastani kati ya asilimia 50.70 na asilimia 92.38.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, shule ya St Francis Girls ilishika nafasi ya kwanza kitaifa ikifuatiwa na Kemebos, Bright Future Girls, Canossa, Tengeru Boys, Centennial Christian, St Monica Moshono Girls, Marian Boys, Precious Blood na Feza Boys


Halmashauri zilizofanya vizuri

Dk Msonde alibainisha pia halmashauri zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne kuwa ni pamoja na Bagamoyo (Pwani), Bukoba (Kagera), Meru (Arusha), Njombe (Njombe), Bariadi (Simiyu), Kibondo (Kigoma), Moshi M (Kilimanjaro), Kibaha (Pwani), Moshi (Kilimanjaro) na Mtwara M (Mtwara). Zilizoongeza ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo ni Madaba (Ruvuma) Liwale (Lindi), Moshi M (Kilimanjaro) Kibaha (Pwani), Nsimbo (Katavi), Tandahimba (Mtwara), Misungwi (Mwanza), Masasi M (Mtwara), Iringa (Iringa) na Kwimba (Mwanza).

Advertisement