Ufaulu darasa la nne waongezeka, wanafunzi 10 bora hawa hapa

Ufaulu darasa la nne waongezeka, wanafunzi 10 bora hawa hapa

Muktasari:

  • Wanafunzi 1,551,599 wamefaulu mtihani wa darasa la nne kati ya wanafunzi 1,704,286 waliofanya mtihani huo.

Dar es Salaam. Wanafunzi 1,551,599 wamefaulu mtihani wa darasa la nne kati ya wanafunzi 1,704,286 waliofanya mtihani huo.

Ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 1.34 ikilinganishwa na kiwango cha ufaulu kwa mwaka uliopita.

Matokeo ya mtihani huo yametangazwa leo Ijumaa Januari 15, 2021 na katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde na kubainisha kuwa wanafunzi hao wamefanya vizuri kwenye masomo yote.

Amesema ufaulu wa chini ni asilimia 70.85 kwenye somo la hesabu huku ufaulu wa juu ukiwa asilimia 95.46 katika somo la uraia.

Katika matokeo hayo orodha ya wanafunzi 10 bora nafasi ya kwanza hadi ya tatu ilichukuliwa na wanafunzi wa shule ya   PeaceLand iliyiko Mwanza.

Jovinia Kamunyila ndiye aliyeibuka mwanafunzi wa kwanza akifuatiwa na Abdulaziz Marwa na Charles Shilugala.

Nafasi ya nne imeshikwa na Maryfaith Minja wa shule ya Imani iliyopo Kilimanjaro.

Nafasi ya tano, sita na saba zimeshikwa na kwa wanafunzi wa  shule ya Graiyaki iliyopo mkoani Mara ambao ni Baraka Mwita, Beatrice Luvunda na Lucy Mwita.

Stela Mshana wa shule ya Shekina ameshika namba nane wakati nafasi ya tisa ikienda kwa Wenseslaus Shayo wa shule ya Imani na dimba kufungwa na Vailet Msuya wa Shekina pia.