Mchungaji akomba mamilioni ya muumini akidai fungu la 10

Muktasari:

  • Mgogoro wa ama ni mkopo au sadaka ya fungu la kumi (zaka) baina ya Mchungaji John Mtuka wa Kimara na muumini wake, Neema Wawa umehitimishwa na Mahakama Kuu ikibainisha ni mkopo unaostahili kurejeshwa.

Moshi. Mgogoro wa ama ni mkopo au sadaka ya fungu la kumi (zaka) baina ya Mchungaji John Mtuka wa Kimara na muumini wake, Neema Wawa umehitimishwa na Mahakama Kuu ikibainisha ni mkopo unaostahili kurejeshwa.

Muumini huyo alimfikisha mahakamani mchungaji huyo akimdai Sh15 milioni alizomkopesha, huku mchungaji huyo akidai fedha hizo hazikuwa mkopo, bali zilitolewa kama sadaka ya fungu la kumi kwenye kanisa wanaloabudu (halikutajwa), shauri ambalo limefika hadi mahakama kuu.

Hata hivyo, katika hukumu yake, Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ya Dar es Salaam, alisema fedha hizo, hazikuwa fungu la kumi wala sadaka ya ujenzi kama mchungaji alivyokuwa anaeleza, bali ulikuwa ni mkopo.

Hayo yamo katika hukumu ya Jaji Nkwabi iliyotolewa juzi kuhusu rufaa ya kesi iliyokuwa imekatwa na Mchungaji Mtuka, akipinga hukumu ya mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ya Agosti 2, 2022 iliyompa ushindi Neema Wawa.

Katika hukumu hiyo, Jaji Nkwabi alianza kwa kusema rufaa hiyo inashangaza kwa sababu wadaawa walikuwa na mahusiano ya mchungaji na muumini na muumini alikuwa akihudhuria kanisani ambako mchungaji aliweza hadi kufahamu ukwasi wake.

“Ilitokea pale uwezo wa kifedha wa mjibu rufaa (Neema) ulipokaa sawa, mrufani (mchungaji) alifahamu kupitia fungu la kumi alilokuwa akilitoa, suala ambalo kiukweli ndiyo mahitaji ya mafundisho ya dini,” alieleza Jaji.

“Wakati mchungaji anadai muumini wake alilipa Sh5 milioni kama fungu la kumi, muumini wake anasema alilipa tu Sh1 milioni kama fungu la 10. Kwa maoni yangu utata wa hii kesi ulianzia hapa, ukichanganya na madai ya michango ya ujenzi,” alisema.
 

Mkopo wa Sh15 milioni

Jaji anasema kulingana na ushahidi wa pande zote mbili ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama, haikupita muda mchungaji alibaini muumini huyo alikuwa na fedha za kutosha kwenye akaunti, akaanza kumuomba amkopeshe.

Mwanzoni muumini huyo alikataa, lakini kutokana na mchungaji kuapa kuwa angemrudishia, alikwenda benki na kutoa Sh18 milioni na kati ya hizo akampa mchungaji Sh15 milioni kama mkopo ambao haukuwa na riba kama ilivyo katika taasisi za fedha.

Baada ya muda wa kurejesha mkopo kupita, Neema alianza kudai arejeshewe fedha zake bila mafanikio na aliwatahadharisha waumini wengine wasije wakaingia kwenye mtego huo.

Baada ya kushindwa kabisa kupata fedha zake, akaamua kwenda kortini.
Katika Mahakama ya Mwanzo Kimara, mahakama iliitupa kesi hiyo kwa maelezo kuwa miamala ya kukopeshana haikuwa katika maandishi.

Hata hivyo, muumini huyo hakuridhika, akakata rufaa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kushinda rufaa hiyo.

Mahakama hiyo iliamuru arejeshewe Sh12 milioni, lakini mchungaji hakuridhika na maamuzi hayo akiegemea sababu tatu; moja ni kuwa mahakama haikuzingatia mahusiano yaliyopo kati ya mchungaji na muumini wake katika kanisa hilo.

Mchungaji huyo alisema kwa kuwa Neema alikuwa muumini wa kanisa hilo, ilimfanya awajibike pia kulipa sadaka ya fungu la kumi au zaka na kutoa michango mbalimbali mingine ya kanisa, kabla ya kubadilika na kuanza kudai arejeshewe.
 

Hukumu Mahakama Kuu

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Nkwabi alisema katika mawasilisho ya rufaa, mchungaji alieleza kuwa muumini wake alitoa Sh5 milioni kama zaka, Sh2 milioni za ujenzi na Sh5 milioni ndio ulikuwa mkopo alioudai baada ya kuhama kanisa lake.

Lakini muumini yeye katika mawasilisho yake alisema mchungaji alitoa mawasilisho ya uongo na kufafanua kuwa alitoa Sh1 milioni tu za zaka na kuwa alimkopesha mchungaji Sh15 milioni alizotakiwa kurejesha ndani ya wiki.

Jaji Nkwabi alisema wakati mchungaji anasema alipewa Sh12 milioni ambazo ni mjumuiko wa fungu la kumi, na michango, shahidi wake alisema alipewa Sh12 milioni kama sadaka ya shukrani na kuzidisha mkanganyiko wa madai.

“Lakini ushahidi wa mjibu rufaa (muumini) alikuwa na msimamo usioyumba kuwa alimpa Sh15 milioni kama mkopo. Naona ushahidi wa mjibu rufaa ndio wa kuaminika. Kwa nini sadaka iende mkono kwa mkono na mkopo?” alihoji Jaji.

“Nimeridhika kwamba kwa mtiririko wa matukio yaliyoelezwa na mjibu rufaa (Neema) ni sahihi na ushahidi wake una uzito kuliko wa mrufani (mchungaji). Kwa kuwa Neema alishalipwa Sh1, 063,000, mrufani atalipa Sh13, 937,000,” alisema Jaji Nkwabi.

Vilevile Jaji alimwamuru mchungaji John kulipa gharama za shauri hilo katika mahakama kuu na mahakama ya wilaya.