Mchungaji wa Congo jela miaka mitatu gerezani
Mshtakiwa Jean Mbunzu ambaye ni mchungaji na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kuhukumiwa. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Jean anadaiwa kutenda makosa yake, Juni 8, 2026 katika ofisi za Uhamiaji, zilizopo Kurasini Jiji Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu mchungaji na raia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Jean Mbunzu (35) kulipa faini ya jumla ya Sh1 milioni au kwenda jela miaka mitatu, baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia kitambulisho cha Taifa (Nida) na kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Uhamiaji.
Mbunzu ametiwa hatiani na mahakama hiyo, baada ya kukiri mashtaka hayo mawili, muda mfupi baada ya kusomewa mashtaka yake.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo, hivyo amepelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo hicho.
Hukumu hiyo, imetolewa leo Juni 17, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Beda Nyaki baada ya mshtakiwa kukiri mashtaka yake ya kughushi nyaraka na kujifanya ni Mtanzania, kinyume cha sheria.
Akitoa uamuzi, Hakimu Nyaki amesema shtaka la kwanza ambalo ni la kutoa taarifa za uongo, mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miaka mitatu.
"Vilevile shtaka la kujipatia kitambulisho cha Taifa (Nida) kinyume cha sheria, Mbunzu atatakiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miaka mitatu na haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hajaridhika na uamuzi" amesema Hakimu Nyaki.
Awali, mawakili wa Serikali Mohamed Mlumba na Ezekiel Kibona, waliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kwa kuwa kitendo hicho hatari kwa usalama wa nchi.
"Mheshimiwa hakimu, tunaiomba mahakama yako tukufu itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyu, kwa sababu kitendo cha kughushi nyaraka na kujipatia kitambulisho cha Nida ni kosa kubwa na hatari kwa usalama wa Taifa" amedai wakili Mlumba
Hata hivyo, Mahakama ilipotoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, aliomba asamehewe makosa yake.
Hakimu baada ya kusikiliza ungamo la mshtakiwa na hoja za upande wa Jamhuri, alimhukumu adhabu hiyo.
Katika kesi ya msingi, mchungaji anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 8, 2026, katika ofisi za Uhamiaji Kurasini jijini Dar es Salaam alipotoa taarifa za uongo kwa maofisa uhamiaji kuwa yeye ni raia wa Tanzania na kufanikiwa kupata kitambulisho cha taifa (Nida) chenye jina la John Francis Maponda, akijua yeye si Mtanzania.
Iliendelea kudaiwa, katika tarehe na eneo hilo, mshtakiwa huyo alibainika kutoa matamko ya uongo kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi kwa maofisa uhamiaji na kufanikiwa kupata kibali cha ukazi daraja C.