Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saba kortini wakidaiwa kuiba lita 2,800 za mafuta

Washtakiwa saba wanaokabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kuiba lita 2,800 za mafuta ya ghafi, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Wanadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya Juni 2, 2026 na Juni 4, 2026, Mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke.

Dar es Salaam. Msimamizi wa tanki la mafuta, Kassim Kongwa (43) na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo kuongoza genge la uhalifu na wizi wa lita 2,800 za mafuta ghafi, yenye thamani ya Sh26 milioni, mali ya Kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Limited.

Washtakiwa wengine ni Hemed Abdallah (30), ambaye ni kibarua wa Kampuni ya Azania, Hassan Kimoge (42), Juma Issah(43), Halfan Halfan, maarufu Ruba, Maria Gulaba ambaye ni opareta wa kiwanda hicho pamoja na mlinzi, Jafar Molel.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Juni 17, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 13513 ya mwaka 2026 na wakili wa Serikali, Winiwa Kasala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Anna Magutu.

Kabla ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Magutu aliwaeleza washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea kusalia rumande hadi upelelezi utakapokamilika.

Hakimu Magutu baada ya kutoa maelekezo hayo, wakili Kasala aliwasomea mashtaka yao.

Amedai, kati ya Juni 2, 2026 na Juni 4, 2026, jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu, washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu na kuiba mafuta ghafi mali ya kampuni hiyo.

Kasala amedai shtaka la pili ni wizi, ambapo Juni 4, 2026 mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke, ambapo watuhumiwa hao waliiba lita 2,800 za mafuta ghafi yenye thamani ya Sh26 milioni, mali ya kampuni hiyo.

Shtaka la tatu ni kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, ambapo katika tarehe hizo na eneo hilo washtakiwa hao walijipatia lita 2,800 za mafuta wakijua mafuta hayo yalitokana na kosa tangulizi la wizi.

Baada wa kuwasomea mashtaka yao, upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi haijakamilika hivyo wanaomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Magutu ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 30, 2026 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.