MCL kushiriki wiki ya ubunifu

MCL yaja na wiki ya ubunifu

Muktasari:

Wadau wa sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia kuanzia leo watakuwa na siku tatu za kupata chakula cha ubongo, kwani watapata fursa ya kusikia mada na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo kwa wakati huu na siku zijazo.

Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia kuanzia leo watakuwa na siku tatu za kupata chakula cha ubongo, kwani watapata fursa ya kusikia mada na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo kwa wakati huu na siku zijazo.

Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) kupitia idara yake ya ubunifu ya Habarihub imeandaa mdahalo kuhusu ubunifu wa kidijatali na tasnia ya habari na hilo ndilo litakuwa jukwaa kwa wadau hao pamoja na wananchi kwa ujumla.

Waandaaji wengine wa kongamano hilo ni Mfuko wa Ubunifu na Maendeleo ya Binadamu (HDIF), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (UKaid), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)

Mdahalo huo utakuwa ukifanyika kwa njia ya mtandao kuanzia saa 8 hadi saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Wataalamu mbalimbali kutoka Marekani, Uingereza, Zambia, Kenya, Uganda na Tanzania watatoa na kuchangia mada.

Akizungumzia mdahalo huo jana uliodhaminiwa na Benki ya Absa Tanzania na Kampuni ya Epiroc Mkuu wa idara ya Habarihub, Wilmore Mihayo alisema kutakuwa na mada tatu ambapo kila siku itakuwa ni mada moja itakayojadiliwa kwa muda wa saa mbili.

Mihayo alisema zitakuwa ni siku tatu kwa ajili ya tasnia ya habari, kwani yataangaziwa mabadiliko ya tasnia hiyo katika suala la teknolojia, biashara na mahitaji ya mlaji sanjari na athari zake katika biashara, uendeshaji wa kila siku na mlaji wa maudhui hayo.

“Tutaanza na mabadiliko ya kimtazamo, elimu na mfumo wa ajira unavyohitaji kuvutia talanta katika karne ya 21, siku inayofuata itakuwa juu ya ukusanyaji wa habari kwa ajili ya majukwaa tofauti na stadi za muhimu kwa mwandishi wa habari wa karne ya 21.

“Siku ya tatu ni juu ya teknolojia muhimu katika mapinduzi ya viwanda ya awamu ya nne na athari zake kwa dunia ya sasa,” alisema Mihayo.

Kwa yeyote atakayependa kushiriki ni bure, lakini ni lazima kujisajili kupitia kiunganishi hiki https://events.habarihub.co.tz/