MCL yaongoza wateule tuzo za EJAT 2022

Waandishi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) walioingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tuzo za EJAT 2022

Muktasari:

  • Jumla ya waandishi 18 wa magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti wameteuliwa kuwania Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2022 na kuwa miongoni mwa wateule 91 kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Dar es Salaam. Jopo la majaji wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) limewateua waaandishi 18 kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuwania tuzo hizo kati ya wanataaluma 91 watakaoshindanishwa katika kilele cha tuzo hilo Julai 22 katika Ukumbi wa Mlimani City.

Akitangaza wateule hao jijini Arusha leo Ijumaa, Juni 23, 2023 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi EJAT 2022, Kajubi Mukajanga amesema waandishi 91 wameteuliwa kati ya 728 waliowasilisha kazi zao.

Amesema kati ya hao 36 wanaandikia magazeti, 27 mitandao ya kijamii na 15 ni kutoka redioni na wanaotokea kwenye runinga ni 15.

Kajubi amewataja waandishi kutoka MCL kuwa ni Ephrahim Bahemu, Peter Elias, Elizabeth Edward, Herieth Makwetta, Julius Mnganga, Kelvin Matandiko, Baraka Loshilaa, Imani Makongoro, Juma Issihaka, Janeth Joseph, Mussa  Juma, George Helahela, Pamela Chilongola, Tumaini Msowoya, Saddam Sadick, Josephine Sebastian, Clezencia Tryphone na Mariam Mbwana.

“Katika wateule wote 44 ni wanawake ambapo 16 kutoka kwneye magazeti, 12 kutoka mitandao ya kijamii, sita kutoka katika redio na 10 ni runingani, wateule wanaume jumla yao ni 47,” amesema Kajubi.

Amemtaja mgeni rasmi katika kilele cha tuzo hizo atakuwa Jaji Othman Chande ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Haki Jinai.

Mwaka 2022, waandishi watano walishinda tuzo sita za Ejat, kati ya waandishi 61 kutoka vyombo mbalimbali vya habari walioingia katika kinyang'anyiro, hicho ambapo MCL iliingiza wateule tisa katika Ejat 2021.