Mdau wa utalii amwagiwa ‘tindikali’ Moshi

Muktasari:

  • Mdau wa utalii na mkazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Tariq Awadhi amedai kumwagiwa kimiminika kinachodhaniwa kuwa tindikali usoni.

  


Moshi. Mdau wa utalii na mkazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Tariq Awadhi amedai kumwagiwa kimiminika kinachodhaniwa kuwa tindikali usoni.

Mwanaume huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) amesema kuwa anadhani aliyemmwagia kimiminika hicho ni mtu wake wa karibu ambaye ni mwanaume.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo amesema kuwa hilo linachunguzwa ili wale waliofanya tukio hilo waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

"Ni kweli hili tukio lipo na Jeshi la Polisi tunalichunguza na mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hili," amesema

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Tariq amesema tukio hilo lilitokea Machi 5 mwaka huu wakati akiwa njaini kwenda kula ndipo walipita vijana wawili wakiwa na bodaboda na walipofika karibu yake walipunguza mwendo wakamwagia kitu usoni.

"Machi 5 mwaka huu nilikuwa nimetokea nyumbani wakati nikiwa barabarani maeneo ya Shant Town ilinipita bodaboda ikiwa na watu wawili baada ya muda kidogo walipunguza mwendo, wakarudi kunifuata lakini muda huo nilikuwa sijashtuaka chochote nilihisi labda ni vibaka, gafla walipita mbele yangu wakiwa wamepunguza mwendo na kunimwagia kitu machoni,"

Waliponimwagia nilipogusa uso kikaanza kunichoma na macho yalifumba nikaanza kupiga kelele kutafuta msaada. Dakika tano nikapata msaada wa mtu wa kunipeleka hospitali, namshukuru Mungu japo sijapona anaendelea kunipigania,"amesema na kuongeza

"Naamini huyu aliyenifanyia hili tukio yupo ni mtu ambaye alikuwa na interest na mimi ndio maana akafanya alichonifanya, kuna jamaa yangu flani hivi alikuwa akinitumia meseji ambazo nilikuwa sizielewi kama mwanaume mwenzangu kutokana na tabia ile nikam'block' visa ndio vikaanza pale,"

"Ni kwanini nikasema ni yeye? ni kwa sababu alishasema huyu mtu nitamharibu sura na nitahakikisha amelala kitandani miaka miwili baada ya kusema hayo ndani ya siku likatokea lililotokea na hii ni kutokana na kwamba nilimpuuza kutokana na mambo yake ya ajabu aliyokuwa akiyataka kutoka kwangu,"

Mpaka sasa Tariq ametimiza zaidi ya mwezi mmoja akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.