Mdee, Naibu Waziri wachuana bungeni

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Halima Mdee akizungumza wakati akichangia makadirio ya mpato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25 leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Baada ya Serikali kutamka kurejesha mikopo ya halmashauri ya asilimia 10, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee ameibuka na hoja ya kutaka ripoti ya kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuangalia utoaji wa mikopo hiyo ipelekwe bungeni ili ijadiliwe.

Dodoma. Utaratibu wa urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri umeibua mjadala kati ya Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange.

Mjadala huo uliokuwa na staili ya kuomba taarifa kwa Dugange, umebuka leo Jumatano Aprili 17, 2024, wakati Mdee alipokuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Tamisemi kwa mwaka 2024/25.

Akichangia, Mdee amesema Serikali imesema imejipanga kufanya marekebisho ya sheria na kanuni zinazosimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 iliyokuwa ikitolewa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu ili kuongeza ufanisi.

Amesema sasa hivi wako katika Bunge la Bajeti na kwamba mchakato wa utoaji mikopo unaanza Julai mosi, mwaka mpya wa fedha.

Hata hivyo, amesema wakati wanakwenda kurejesha mikopo hiyo, Tamisemi bado haijarekebisha sheria, kanuni wala taratibu ambazo zinatarajiwa kusimamia mchakato huo.

Amesema hotuba ya Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa inaonyesha wamekurupuka katika suala hilo na wala hawajajiandaa, ndio maana hawana sheria wala kanuni zinazosimamia mikopo hiyo.

“Waziri kwa makusudi najua hujaandika chochote kuhusiana na mikopo chechefu na mimi najua fedha za wananchi lazima zikaguliwe, huwezi kufunika kombe ili mwanaharamu apite,” amesema.

Amesema Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22 ilionyesha katika halmashauri 184 nchini, mikopo yenye thamani ya Sh88 bilioni ilikuwa haijarejeshwa.

Amesema ripoti hiyo ndio iliyosababisha kusitishwa kwa muda kwa mikopo hiyo.

Amesema wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitangaza kusitishwa kwa mikopo hiyo mwaka 2023, alisema wamefanya hivyo ili kuunda kikosi cha wataalamu kitakachotoa mapendekezo ya utoaji wa mikopo na urejeshwaji.

Mdee amesema Majaliwa alisema bungeni kamati hiyo itakapokamilisha kazi itawasilisha ripoti yake kwa wabunge na wananchi ili kupata uelewa wa pamoja kuhusu mikopo hiyo.

“Leo mwaka mmoja baadaye, tunakuja kusomewa katika hotuba vitu ambavyo havieleweki bila kujua kikosi kazi kilichofanya kazi kiligundua nini, changamoto ni nini, tunaelekea mbele kivipi,” amesema.

Amesema Aprili 2023 aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, (Angellah Kairuki ambaye sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii) alitoa maelekezo kwa wakurugenzi ndani ya miezi mitatu, Sh88 bilioni ambazo ni mikopo chechefu ziwe zimekusanywa zote na kurejeshwa serikalini.

“Julai (mwaka jana) hadi tunaahirisha Bunge hakusema kitu, mwaka mmoja baadaye hakuna kitu ambacho kimefanyika,” amesema.

Hata hivyo, Dk Dugange alimpa taarifa kuwa baada ya kusitisha mikopo hiyo Aprili mwaka jana, kamati ilifanya kazi yake na kupeleka ripoti ambayo iliwawezesha kugundua sababu za uwepo wa mikopo chechefu.

Amesema sababu hizo ndizo zilizotumika kuandaa mpango mpya ambao utaanza Julai 2024 na kwamba hadi Machi 30, 2024 mikopo yenye thamani ya Sh63 bilioni zilikuwa zimerejeshwa.

Akiendelea kuchangia, Halima amewataka mawaziri kusikiliza na kutumia muda wao wa kujibu hoja za wabunge badala ya kutoa taarifa wakati wakichangia.

Mdee amesema Majaliwa aliahidi kuleta ripoti hiyo bungeni ili wabunge waweze kujadili na kutoa ushauri utakaoepusha changamoto zilizojitokeza awali kujirudia.

“Mnatoka huko mnakuja kutupa hotuba ya jumla jumla ambayo haieleweki. Kwa nini tunasema haieleweki ni kuwa hii sheria tunayoitekeleza ina kanuni zake za mwaka 2019,” amesema.

Amesema katika kanuni ambazo zimewafikisha katika changamoto hizo kulikuwa na utambuzi wa vikundi kuanzia ngazi ya mtendaji wa kijiji, kata, mkurugenzi na menejimenti yake, kamati ya fedha ya halmashauri hizo, mabaraza ya madiwani, Tamisemi na kisha mikoa.

“Sasa kama mlifeli katika muktadha huu kwa nini hamkuleta hizo findings (matokeo ya utafiti) ili tujue kinagaubaga,” amehoji.

Amesema katika ripoti ya CAG aliyoitoa Machi 2024, ukurasa 103 anasema mikopo ambayo haijarejeshwa kutoka katika vikundi ni Sh79.76 bilioni.

Mdee amesema CAG amechambua katika ripoti yake halmashauri 149 kati ya halmashauri 184 zina mikopo ya muda mrefu yenye thamani ya Sh79.7 bilioni.

Amesema hiyo inamaanisha katika mwaka wote wameweza kurejesha Sh8 biloni tu.

Mdee amesema CAG alisema kwenye mikopo mipya ya mwaka 2022/23, jumla ya Sh75 bilioni ziligawia kwa wananchi lakini mikopo iliyotakiwa kurejeshwa katika kipindi hicho yenye thamani ya Sh27.6 bilioni haikurejeshwa.

Amesema hiyo inafanya jumla ya mikopo isiyorejeshwa ni Sh107 bilioni na kwamba utaratibu mpya ambao unakwenda kuanza Julai mwaka huu, hauna tofauti na ule wa awali.

Mdee ametoa mfano wa Halmashauri ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambayo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh15 bilioni lakini zaidi ya Sh6.2 bilioni hazijarejeshwa.

Hata hivyo, Dk Dugange alimpa taarifa Mdee kuwa marejeo aliyoyafanya (Mdee) ya mikopo ya mwaka 2022/23, si mikopo yote inayorejeshwa ndani ya mwaka mmoja wa fedha.

“Kwa hiyo kuna mikopo ambayo muda wake wa kuiva bado haujafika na Serikali itaendelea ku-recover (kuboresha) mikopo hiyo. Lakini utaratibu wa sasa sio sawa na utaratibu uliopita ndio maana kuna ajira za maofisa maendeleo,”amesema.

Amesema kutakuwa na kamati za mikopo za vijiji, kata, tarafa za wilaya na za mikoa lakini pia wameajiri wataalamu wengi na hivyo anamhakikishia kuwa utaratibu wa sasa utakuwa bora zaidi.

Akiendelea kuchangia, Mdee amemtaka Dk Dugange akarejee kwenye kanuni za sasa kwa sababu alivyovisema vimo ndani ya kanuni hizo na kwamba tatizo ni watu wengi hawana utaratibu wa kusoma.

Jana, akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi bungeni, Waziri  Mchengerwa amesema wamerejesha utoaji wa mikopo hiyo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kuanzia Julai 2024 kwa utaratibu wa kutumia benki kwa halmashauri 10 za majaribio.

Alizitaja halmashauri hizo ni za majiji ya Dar es Salaam, Dodoma, manispaa za Kigoma Ujiji na Songea na miji ya Newala na Mbulu pamoja na Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.