Chadema yafunga jalada kina Mdee

Wafuasi wa Chadema wakiwa katika maandamano ya amani yaliyofanyika jijini wa Mwanza leo Februari 15 2024. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amewatajia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara namba za simu za Spika  Tulia Ackson akiwaambia watumie madaraka na mamlaka yao ya kikatiba na kiraia kuiwajibisha Serikali juu ya kuwakingia kifua wabunge hao

Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekabidhi hatima ya wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa kwenye chama hicho kwa wananchi, kikidai kimetumia kila aina ya njia ya kiofisi kuwaondoa bungeni bila mafanikio.

Wabunge hao waliingia bungeni baada ya kuapishwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai Novemba 24, 2020 katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.

Baada ya kuapishwa walivuliwa uanachama na chama hicho wakidaiwa kukiuka katiba na kanuni za Chadema, kwa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu bila kupitishwa na chama.

Hata hivyo, wabunge hao walifungua shauri mahakamani kupinga kuvuliwa uanachama, wakidai hawajasikilizwa.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 15 kwenye mkutano wa hadhara wakati wa kuhitimisha maandamano ya amani kwenye uwanja wa Furahisha, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema pamoja na kufuata taratibu zote za kiofisi lengo hilo limekwama.

Katibu huyo amewatajia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo namba za simu za Spika Dk Tulia Ackson akiwaambia watumie madaraka na mamlaka yao ya kikatiba na kiraia kuiwajibisha Serikali juu ya kuwakingia kifua wabunge hao.

“Najua wapo watakaosema kwa nini umefanya hivyo, nataka niwaambie tumetumia kila njia za kawaida za kiofisi kumtaka spika ajibu barua na achukue hatua tangu Novemba, 2020. Kama Spika anashindwa kukiheshimu chama kikuu cha

upinzani tangu tulipopeleka barua kwa mara ya kwanza na kumkumbusha kwa miaka kadhaa, jambo hili sasa lipo kwenu wananchi ambao madaraka na mamlaka yapo kwenu ya kuiwajibisha Serikali na viongozi wake. Chukueni hatua ambazo mnaona zinafaa kwa mujibu wa sheria, Katiba na hata haki zenu za kiraia,” amesema Mnyika

Amesema Desemba 15, 2023 Mahakama ilipotoa hukumu ya kesi ilisema maamuzi ya Kamati Kuu ya chama ya kuwafukuza wabunge 19 uanachama yalikuwa halali, baada ya uamuzi aliandika barua kwa Spika kumjulisha hakuna kesi mahakamani, hivyo  inatakiwa kuwaondoa bungeni.


Amvaa Makonda

Mnyika amesema ujio wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda na mbinu mpya ya kutatua kero za wananchi jukwaani na kuwavaa watendaji wa umma, ni ya kuitenganisha Serikali na CCM jambo ambalo amedai Serikali iliyoko madarakani na chama tawala haviwezi kutenganishwa.

“Tunawaomba wananchi hawa CCM wapuuzwe na tuendelee na maandamano, mpaka wasikie sauti ya umma,” amesisitiza.


Msimamo wa Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wameandamana kwa kutembea kwa zaidi ya kilomita 45 kwenye njia zote tatu za Buhongwa, Igoma na Ilemela Kanisani ili kupaza sauti kwa Serikali, huku akimkaribisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa na wakili Boniface Mwabukusi Chadema.

“Na sisi ndani ya Chadema tumesema hatuna rafiki wa kudumu au adui wa kudumu, ila ambacho ni cha kudumu ni masilahi ya nchi. Na ndiyo maana leo katika uwanja huu tunaye katibu mkuu wangu wa zamani, Wilbroad Slaa, msiniulize sasa hivi yuko wapi, lakini kama yuko hapa yuko Chadema. Sisi hatuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu karibu Chadema tufanye kazi,” amemwambia Dk Slaa.

Amesema yeye na viongozi wenzake baada ya kumaliza mkutano huo wataelekea Monduli kumstiri aliyekuwa Waziri Mkuu na mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akisema wanatambua mchango wake.

“Ndugu zangu Taifa lina msiba kwa kumpoteza Lowassa, aliamua kuja Chadema baada ya kuonewa CCM. Tumefanya naye kazi kwa miaka mitatu alikuwa na mchango wa kuijenga Chadema. Pamoja na kwamba alirudi CCM hatuwezi kuogopa kusema kwamba alikuwa na mchango wa kuijenga Chadema, ndiyo maana tulisema tutaomboleza kwa kufanya maandamano,” amesema.

Mbowe amesema chama hicho kitaendelea kusimamia mambo manne ambayo ni haki za watu kupitia tume huru, Katiba mpya, uhuru, demokrasia na maendeleo ya watu.

“Kelele tunazopiga tunalenga kujenga misingi ambayo viongozi wanapatikana kwa njia za demokrasia kwa misingi ya maamuzi ya wapiga kura. Yeyote anayepata ofisi ya umma awe amepata ridhaa ya wananchi, kazi zote za siasa tutakazofanya zichangie katika maendeleo ya kweli ya watu wetu. Watanzania wengi bado ni masikini na umasikini unaongezeka, viongozi tulionao hawana uwezo wa kututoa kwenye umasikini,” amesema.

Amesema kutokana na nguvu ya umma ipo siku Serikali itawaomba warudi mezani kuzungumza na hawatakuwa wapole.

Akizungumza katika mkutano huo, Dk Slaa aliyesema anawakilisha Taasisi ya Sauti ya Watanzania, ameeleza kuwa  amehudhuria maandamano hayo kuwakilisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) na wanaoishi nchini wenye hasira na Serikali kutokana na kukanyaga Katiba
“Kazi ya ukombozi ni ya kwetu sote. Mheshimiwa mwenyekiti tutaendelea kuwaunga mkono katika yote mnayofanya… tutashirikiana kwa sababu ajenda ya kukomboa nchi ni ya Watanzania wote,”amesema Mbowe.


Lissu adai kuchoshwa

Makamu Mwenyekiti wa Chadema -Bara, Tundu Lissu alisema licha ya maandamano hayo kuwachosha kimwili lakini nafsi zao zimetakata kwa kuwa wamefikisha ujumbe waliokuwa wameukusudia serikalini, akidai wamechoshwa na mambo yanayoendelea ikiwemo kodi, tozo na ushuru unaonyonya wananchi.

Lissu amesema wamechoshwa kunyang’anywa maeneo ya biashara, ya kilimo, ya makazi na ya ufugaji.

Amesema wavuvi wamechoka kunyanyaswa waingiapo ziwani, wamechoshwa fedha za umma na rasilimali kuibwa, hata kuibwa kura za chaguzi kuanzia kwa wenyeviti wa mitaa, madiwani, wabunge na hata ule wa urais.

Amedai wanaibiwa kura kwa sababu ya uandikishwaji wa wapigakura kuwa mbovu, akidai wapigakura wengine huachwa kwa sabau ya ya kazi kufanywa kwa haraka, huku Wazanzibari wakiandikishwa kwa masharti likiwemo kutakiwa kukaa mahali kwao kwa miaka mitatu.

 “Hata kampeni za uchaguzi ni za ovyo zinaharibu uchaguzi ikiwemo wagombea kufungiwa, kupigwa mabomu. Tunaibiwa uchaguzi siku ya uchaguzi wenyewe mawakala wetu hawaapishwi, hawaruhusiwi kuingia vituoni, hivyo madai ya Katiba mpya ni muhimu,” amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chadema (Bavicha), John Pambalu amewakejeli baadhi ya watu aliodai hawajihusishi na siasa akiwaambia licha ya kujitenga lakini nao wanaonja joto la mfumuko wa bei na ugumu wa maisha.

“Wapo waliokuwa wakisema siasa haituhusu, imewahusu kwenye kilo ya sukari, walisema siasa haituhusu na ni vinyozi wameiona imewahusu kwenye mgao wa umeme, walisema siasa haiwahusu imewahusu kwenye kikokotoo, hayupo aliyebaki salama,” alisema Pambalu.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche alisema maandamano hayo yanatoa ujumbe kwa Serikali kuwa wananchi wanachukia kutokana na hali ngumu ya maisha na mambo mengine yanayoendelea nchini.

“Ndugu zangu nawashukuru kwa kujitokeza. Mmetembea zaidi ya kilomita 20 kutoka Buhongwa, kilomita 15 kutoka Igoma, tunataka kumwambia Rais Samia maandamano si harusi, hatuandamani kwa sababu tuna furaha tunaandamana kwa sababu tumechukia,” amesema.

Wakili Mwabukusi amesema harakati na maandamano yanayoitishwa na Chadema yanalenga kuondoa mfumo wa umwinyi ambao watu wachache wanafurahia rasilimali za nchi.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Kenani, amedokeza kuanzisha mchakato na kupeleka barua kwa Katibu wa Bunge kwa kusudio la Katiba mpya.

“Nitaipigania Katiba mpya ndani ya Bunge na leo niko nje kupigania nje ya Bunge,’’ amesema Kenani.

Mbunge atakayechaguliwa na Katiba mpya hatokubali wananchi wateseke amekaa bungeni,” amesema.

Aliyekuwa mbunge wa Nyamagana na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje ametaja sababu nyingine ya kuandamana hasa kundi la vijana ni kutokana ukosefu wa ajira licha ya kusoma na kupata ujuzi katika fani mbalimbali, hivyo kuishia kuwa madereva bodaboda.

“Leo tumetoka jasho kuandamana kupigania vijana kama hawa ambao ndoto zao za kuwa madaktari, za kuwa mtu katika maisha inateketezwa na Chama cha Mapinduzi,” amesema.

(Imeandikwa na Saada Amir, Mgongo Kaitira, Damian Masyenene na Anania Kajuni)