Mdogo wake Mwalimu Nyerere muasisi Dodoma kuwa makao makuu

Rais Samia, Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla pamoja na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete katika uzinduzi wa Ikulu ya Chamwino leo Jumamosi Mei 20, 2023 jijini Dodoma.

What you need to know:

  • Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi huo ilifanyika Mei 30, 2020, tukio ambalo lilishushuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza historia ya uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya nchi kwenda Dodoma, huku akieleza kwamba uamuzi huo umekamilika kutokana na jitihada za awamu zote za uongozi wa nchi.

Rais Samia amebainisha hayo leo Mei 20, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ikulu ya Chamwino, Dodoma iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na wastaafu wa awamu zilizopita.

Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Rais Samia amesema mchakato wa kuhamishia makao makuu Dodoma ulianza muda mrefu na ulipita katika ngazi mbalimbali za chama na baadaye kutangazwa.

Mkuu huyo wa nchi alisema historia inaeleza kwamba mwaka 1966, Joseph Nyerere, mdogo wake Mwalimu Nyerere, aliwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka Dodoma iwe makao makuu ya nchi.

Hata hivyo, amesema hoja hiyo ilipingwa na wabunge. Pendekezo hilo liliwasilishwa pia ndani ya chama na mwalimu Nyerere akasema ili pendekezo hilo lipitishwe, sharti liungwe mkono wa matawi mengi nchi nzima.

Rais Samia amesema tangu mwaka 1973 Mwalimu Nyerere alipotangaza umma uamuzi kuufanya mji wa Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, kazi ya kuuendeleza mji huo ilianza ili kuufanya uwe na hadhi ya makao makuu ya Serikali.

“Kazi hiyo haikuwa rahisi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kuifanya safari hiyo kuwa ndefu kuliko ilivyopangwa.

“Tangu mwaka 1973 hadi leo mwaka 2023, ni kama miaka 50 hivi badala ya miaka 10 na huu ni umri wa wengi mliomo humu ukumbini,” amesema Rais Samia wakati wa hotuba yake.

“Kazi ilikuwa ngumu na ilikuwa ni jukumu la kila awamu iliyoingia madarakani kuwezesha kuanza ujenzi wa vitu mbalimbali ili Dodoma ichukue sura ya kuwa makao makuu ya serikali. Nawapongeza sana viongozi wa awamu zote kwa jitihada hizi zilizochukuliwa,” amesema.

Ni katika awamu ya tano ya Hayati John Magufuli, uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma ulipopewamsukumo Zaidi. Mtakumbuka Julai 23, 2016, Hayati Magufuli aliukumbusha mkutano mkuu wa CCM kuhusu uamuzi wa kuhamisha rasmi shughuli za serikali kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma

Baada ya hapo utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya jiji la Dodoma uliendelea kwa kasi zaidi ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Dodoma. Eneo hili liliongezwa kutoka ekari 66 hadi kufikia ekari 8,473 na ndipo ujenzi wa jengo hili jipya kuanza na hii leo tunalizindua

“Ujenzi wa Ikulu ya Dodoma ni mradi wa pili kuukamilisha kati ya ile niliyoipokea kutoka kwa Hayati John Magufuli, mradi wa kwanza kuukamilisha ulikuwa ni daraja la Tanzanite. Inshallah Mungu anipe uwezo niikamilishe yote,” amesema Rais Samia.