Meena: Tafsiri ya ‘mwandishi wa habari’ iangaliwe upya katika sheria

Muktasari:

Wakati serikali ikipokea maoni ya wadau mbalimbali kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yam waka 2016, mjumbe wa kamati tendaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Neville Meena amesema kuna haja ya kufanyia mabadiliko maana ya neno “mwandishi wa habari” katika sheria hiyo.

Dar es Salaam. Mjumbe wa kamati tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TE), Neville Meena amesema kuna haja ya kufanyia mabadiliko maana ya neno “mwandishi wa habari” katika Sheria ya Huduma za Habari yam waka 2016.

Meena ameeleza hayo leo Alhamisi Agosti 11, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kituo cha Radio ya Upendo (Upendo FM) kuhusu mabadiliko ya baadhi ya vifungu katika sheria hiyo kama yanavyopendekezwa na wadau.

Amesema katika Sheria ya Huduma za Habari, kuna maeneo 20 ambayo yanahitaji marekebisho ili kuifanya sheria hiyo kuwa rafiki kwa wadau wa tasnia ya habari lakini pia kwa maendeleo ya taifa.

Moja ya maeneo hayo, amesema ni tafsiri ya neno mwandishi wa habari.

Amesema sheria hiyo ni ya kwanza kutambua kwamba waandishi wa habari wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ni taaluma ya uandishi wa habari, hata hivyo amesema tafsiri yake kwenye sheria hiyo ni finyu.

“Kwa hiyo, sisi tunapendekeza tuzingatie pia inhouse training (kujifunza ndani ya vyombo vya habari). Leo vyombo vya habari vya Uingereza wanaamini kwamba wanaweza kumleta mtu yoyote aliyesoma taaluma yoyote ndani ya chumba cha habari, akawa mwandishi, akawa mwandishi mwandamizi, akafikia ngazi ya kuwa mhariri,” amesema.

Meena amebainisha uzoefu unaonyesha wapo waandishi wa habari waliosomea taaluma nyingine lakini wakawa waandishi wa habari wazuri na pia wapo waandishi wa habari waliosomea taaluma hiyo.

Amesema wapo watu ambao hawakuwa na taaluma ya uandishi wa habari lakini walikuja kuwa waandishi wazuri wa habari hadi kufikia ngazi ya uhariri, aliwataja baadhi yao kama vile Absalom Kibanda, Jesse Kwayu na Joseph Kulangwa.

“Tunataka sheria ya habari itambue mfumo wa pili ambao utawawezesha watu wasiosomea uandishi wa habari, kuwa waandishi wa habari kwa kuzingatia tu kwamba wana elimu ambayo inaweza kuwa inakidhi vigezo au viwango vya kufanya kazi katika vyumba vya habari,” amesema.

Mbali na tafsiri ya neno mwandishi wa habari, Meena amesema kuna haja pia ya kuangalia usajili wa magazeti kila mwaka.

Amesema Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo ilifutwa ilikuwa imetoa utaratibu wa usajili, siyo kutoa leseni.

“Usajili ni mara moja, sasa unaweza kusajili lakini ukawa unalipa ada kila mwaka, sasa hapa upo utaratibu wa kutoa leseni kila mwaka, yaani magazeti ikifika Januari Mosi mnaenda kuchukua leseni mpya.

“Unatoa leseni kwa kampuni, unatoa leseni kwa gazeti kila mwaka mpaka Sh1 milioni moja. Kila siku serikali inapiga kelele waandishi wa habari walipwe, sasa hizo hela zinatoka wapi wakati zinasajilia magazeti? Kampuni yenye magazeti matatu kama Mwananchi, lazima walipe Sh3 milioni,” amesema Meena.

Meena amebainisha hayo wakati majadiliano ya wadau kuhusu marekebisho ya vifungu vya sheria ya Huduma za Habari, yameanza leo kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari.