Meno ya tembo, kiboko yamtupa jela miaka 20
Mshtakiwa Abubakari Msangi, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kumiliki meno saba ya tembo na kiboko. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Mshtakiwa amekutwa na vipande hivyo bila kibali, huku akiomba apunguziwe adhabu kwa sababu ana saratani ya jicho.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara, Abubakari Msangi (48) kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kumiliki meno ya tembo na kiboko yenye thamani ya Sh41 milioni, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Julai 17, 2025, na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, aliyesema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa.
Msangi alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kumiliki na kukutwa na nyara hizo. Pia, ametiwa hatiani katika mashtaka mawili ambayo ni kukutwa na na kumiliki nyara hizo.
Hakimu Mwankuga amesema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielelezo vitano, ambavyo vimethibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Pancrasia Protas, aliiomba Mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria kwa sababu utalii ni moja kati ya vyanzo vya mapato kwa Serikali, hivyo kuua wanyama kunahatarisha sekta hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mahakama ilimpa nafasi Msangi kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, naye aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa anasumbuliwa na saratani ya jicho.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba Mahakama yako inipunguzie adhabu kwa sababu nasumbuliwa na saratani ya jicho, pili, nina familia inayonitegemea na nina mtoto yatima anayenitegemea ambaye yupo kidato cha kwanza,” amedai Msangi.
Hakimu Mwankuga amesema kulingana na shufaa alizotoa mshtakiwa na upande wa mashtaka, Mahakama hiyo inampa adhabu ndogo.
“Mahakama imemtia hatiani kama alivyoshtakiwa na kwa kesi hii, adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 20 jela, hivyo Mahakama inamhukumu kila kosa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela,” amesema.
Hata hivyo, Mwankuga amesema adhabu hiyo inakwenda kwa pamoja, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 20 jela ili iwe fundisho.
Kesi ya msingi
Hakimu amesema katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa Oktoba 16, 2020, eneo la Mbagala, aliongoza genge la uhalifu.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, alikutwa na vipande saba vya meno ya tembo yenye thamani ya Dola za Marekani 15,000 sawa na Sh34.293 milioni, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mshtakiwa anadaiwa kukutwa na vipande hivyo bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la tatu, siku na eneo hilo, alikutwa na meno saba ya kiboko yenye thamani ya Dola 3,000, sawa na Sh6.858 milioni, mali ya Serikali.