Mfumo dume unavyowatesa wanawake walima mpunga Mbarali

Wakulima wa mpunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambao wamefikia hatua ya kuvuna, wakipatiwa elimu ya kudhibiti upotevu  shambani  kutoka kwa  wataalamu wa kilimo wa  Taasisi ya Utafiti ya Kilimo (TARI)  .Picha Hawa Mathias

Muktasari:

  •  Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Igurusi, wilayani humo,  asilimia 75 hadi 80 ya wanawake wanajishughulisha na kilimo, lakini wanapofika wakati wa kuvuna na kuuza mazao yao, hutengwa na kutopewa nafasi au haki sawa na wanaume.

Mbeya. Wanawake wa Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, wanajishughulisha na kilimo cha mpunga wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mfumo dume unaozua migogoro inayowasababishia vipigo na ukatili mwingine wa kijinsia.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Igurusi, wilayani humo, Casmiri Pius, asilimia 75 hadi 80 ya wanawake wanajishughulisha na kilimo, lakini wanapofika wakati wa kuvuna na kuuza mazao yao, hutengwa na kutopewa nafasi au haki sawa na wanaume.

Migogoro hiyo mara nyingi huibuka wakati wa msimu wa mavuno, wanaume huchukua jukumu kuu la kusimamia uvunaji na uuzaji wa mazao bila kushirikisha wanawake. Hii inachangiwa na mtazamo dume unaowafanya wanaume wahisi wao ndio wenye mamlaka yote na wanawake hawana sauti katika uamuzi wa kilimo na biashara zake.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Digital umethibitisha kuwa mahusiano ndani ya ndoa yanachangia katika kuchochea ukatili wa kisaikolojia na wanawake wengi hawajui haki zao za umiliki.

Kwa mfano, Teodora Matatala, mkazi wa kijiji cha Mahenje, ambaye ni mama wa watoto watatu, amekumbana na visa vya ukatili, ikiwa ni pamoja na kupigwa na kulazwa jikoni baada ya mume wake kuuza mazao ambayo walilima pamoja na hata kudiriki kuoa mke wa pili.

Teodora amesema walipoanza kilimo mwaka 1997, walipata mafanikio makubwa, lakini mwaka 2000 mambo yalianza kubadilika baada ya mume wake kuanza kufanya uamuzi wa kilimo peke yake na hata kuchukua hatua za ndoa bila kumshirikisha.

Theodora Matatala, akizungumza na Mwananchi kuhusiana na vitendo vya mfumo dume alivyofanyiwa na mumeee baada ya kuzalisha mazao na kuuza.  Picha na Hawa Mathias


Mikasa, vipigo

Amesema baada ya kurejea nyumbani aliwaacha na mke mwenzie, siku ya pili walikuja nyumbani wakiwa wameambatana, walimtaka awapishe chumbani walale, jambo ambalo alitii kwa kuwa alikuwa na nidhamu ya mapenzi kwake. 

Teodora amesema aliona ni vyema kuepusha shari, aliwapisha chumbani na yeye kwenda kulala sebuleni na hakuwa na  sababu ya kukimbia nyumba.

"Siku iliyofuata niliamshwa alfajiri na mume wangu kunitaka kuwaandalia maji ya kuoga, jambo ambalo pia sikusita nikafanya hivyo sambamba na kuwandalia chai, ..baada ya hapo alinitaka kumpatia kaisi cha fedha ambazo tuliuza viazi, nilipokataa alinipiga sana mpaka nikapoteza fahamu na kushtuka nipo hosptalini  na kisha yeye kukimbia,” amesema.

Amesema baada miezi kadhaa mumewe alirejeaa nyumbani na kumuomba msamaha,  huku akimueleza hatorudiana na mke aliyemuoa na kumfanyia vituko vya kumdhihaki, kumpiga na kumtelekeza na familia.

Amesema alipomkea na wakati huo mumewe alikuwa amepigika imaisha, walifanya mipango yao akampatia  mtaji  wa kuuza mbao kijijini hapo.

Amesema kuwa mapenzi yao yalirejea  kuwa ya moto, waliamua tena kulima mpunga hekari  tisa,  lakini  ulipofika wakati wa kuvuna mumewe alimgeuka aliuza mazao peke yake na kumtelekeza na watoto tangu mwaka 2003.

Amesema maisha yake yalikuwa magumu, lakini anamshukuru Mungu alijipambania, sasa anaendelea na kilimo ambapo kwa mwaka huu amelima mpunga hekari tatu na mahindi hekari tatu.

Alirejea kwenye kilimo baada ya ndugu na jamaa kumsihi alime mpunga kwa kujisaidia mbegu na fedha kiasi kwa ajili ya mbolea na viti vingine, huku akiwa amemuacha na watoto watatu.


Wanawake wafunguka

Mkulima wa kijiji cha Maendeleo mfanyabishara wa mchele, Eva Mwandanga amesema ukatili wanaofanyiwa na wanaume umewabadilisha, hali inayosababisha wakivuna mazao wafiche gharani mpaka wakati wa kuuza utakapofika.

Ametaja miongoni mwa ukatili aliofanyiwa ni pamoja na kuzalishwa na kutekelezwa na watoto, ikiwepo wanaume kukosa uaminifu wa utunzaji wa rasilimali fedha ambazo wanachuma pamoja.


Amesema hali hiyo ilimuathiri kwa kiasi kikubwa, jambo lililomfanya kutohitaji tena kuishi na mwanaume na kuendesha maisha yake binafsi.


“Wanaume ndio wametuamsha wanawake, awali tumepitia vipindi vigumu wakati wa kulima tunakuwa sote ikifika kuvuna, mwanamke anakuwa hana haki na kujikuta kuishia kwenye vipigo, kutelekezewa familia, lakini fedha zikiisha wanarejea na tunawapokea, ” amesema.


Mume aliuza mazao

Naye Mkulima wa Mpunga kijiji cha Mswiswi, Recho Fredy amesema mwaka 2022 alikopa fedha za moto "maisha dam"  Sh700,000 kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo kwa kumshirikisha mume wake na  walifanikiwa kuvuna gunia 15.


Amesema baada ya kuvuna na kuhifadhi ndani alipata changamoto, aliposafiri ndipo mume wake aliuza gunia 10 kuhama kwenda kuishi na mwanamke mwingine, huku akimuachia mzigo wa deni la kurejesha mkopo.


“Deni liliendelea kuongezeka  mpaka kufika milioni 1.2, ikiwa ni  riba nikalazimika kutafuta vibarua vya kupiga mpunga na kulima mashamba na kulipwa   ujira wa Sh 10,000 mpaka 15,000 kwa siku ndipo niliendelea kulipa kidogo  kidogo,” amesema.

Amesema kipindi hicho  alipitia maisha ya tabu, kwani mumewe alihama nyumba kwa na kumtelekeza na familia ya  mtoto  wa mwaka mmoja.


Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Igurusi, Casmiri Pius akizungumza na mwandishi wa habari kuhusiana na matukio ya ukatili. Picha na Hawa Mathias

Kauli ya Serikali

Ofisa Ustawi wa jamii Kata ya Igurusi, anayesimamia vijiji tisa, Casmiri Pius amesema bado kuna changamoto kubwa ya matukio ya mfumo dume unaosababisha wanawake kutokuwa na haki ya umiliki, licha ya ushiriki kwenye uzalishaji.


Amesema   asilimia 75 mpaka 80 ya wanawake kazi yao kubwa ni kilimo cha mpunga na kuuza mchele, hivyo kusababisha kuwa na uchumi mkubwa tofauti na wenza wao.

"Kwa takwimu za mashauri ya kesi zilizofikishwa  kwa mwaka 2022 zilikuwa kesi 242 ambapo kwa mwaka 2023 kesi 203 huku kesi 13 zilishauriwa na kufanya upatanishi na ndoa zimeendelea,” amesema.

Amesema asilimia kubwa yanayopokea kipindi cha mavuno na kuuza mazao, kwani kuna wanaume wamekuwa sio waaminifu wamekuwa wakitafuta wateja kuuza na kukimbia famiia kwenda kutumia fedha na ‘michepuko’.


Sababu ya vipigo

 Pius amesema sababu nyingi zinachangia vipigo kwa wanawake kumekuwepo na changamoto kwa baadhi yao  kuwa na dharau kwa wenza wao pindi wanapokuwa na uchumi mzuri.

"Asilimia kubwa wanawake wanamiliki mashamba yao binafsi kutokana na matukio ya mfumo dume inapofika wakati ameuza mpunga wanaanza kuleta dharau kwa wenza wao na kujikuta kuleta migogoro ikiwepo vipigo," amesema.


Mikakati kupunguza mfumo dume

Amesema wameanza mpango wa kutoa elimu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, dawati la jinsia ya kupinga ukatili  dhidi kwa wanawake na watoto.


Amesema wamekuwa wakitoa elimu ya mahusiano katika ndoa namna ya kutoa taarifa za ukatili, migogoro katika ngazi ya jamii na familia  na kwamba wamewafikia watu zaidi 576 katika baadhi ya vijiji na kata.

Amesema wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara ya mara kwa mara kwa kuhusiana viongozi wa vijiji, maofisa maendeleo ya jamii,U ustawi wa jamii na dawati la jinsia la Jeshi la Polisi.

Pius amesema hatua hiyo imekuwa mwarobaini wa kupunguza ukatili miongoni mwa jamii siku hadi siku na kuona ofisi za Serikali ni kimbilio tofauti na miaka ya nyuma.


Wanaume wafunguka

Mkulima Kenneth Ndingo, amesema siku za nyuma walikuwa hawatambui umuhimu wa mwanamke kushiriki kwenye umiliki wa mazao na fedha na badala yake kila jambo linafanywa na mwanaume.

“Ni kweli tulikuwa tukiuza mazao, mama ndani hana sauti anasimamia mwanaume kuuza na  hata kufikia wakati kutelekeza familia kwa kuongeza mke mwingine, fedha zikiisha narudi nyumbani kwenye familia yangu.


“Ilikuwa ukiuza mazao unaongeza mke wa kula naye starehe pesa zikiisha unarejea nyumbani na kumuomba radhi mwenza wangu anakusamehe, kwani wanawake wa mioyo ya huruma sana,” amesema.


Hali ilivyo sasa

Amesema kwa miaka ya sasa wanawake wameamka na kulima mashamba yao na wanapovuna mazao wanahifadhi kwenye maghara na kuacha kuhifadhi majumbani, ili kukwepa mfumo dume.

“Kwa sasa maisha yamebadilika, kila mmoja analima mashamba yake na  akivuna pesa hatuonyeshani  tofauti na miaka ya nyuma tulikuwa tukishirikishana, lakini sasa wanaume ndio tunakumbwa na mfumo jike,” amesema.


Mkurugenzi anasemaje?

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali, Missana Kwangura amesema licha ya kuwa na utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi, idadi kubwa ya malalamiko ni migogoro ya ardhi.

“Changamoto ya mfumo dume zipo, lakini kuna utaratibu ambao unafanywa kwenye ngazi za kata na vijiji kukaa na kumaliza mashauri huko, jambo ambalo linapunguza ukubwa wa tatizo kila kukicha,” amesema.

Imeandikwa kwa ufadhili wa Bill & Melinda Gates Foundation