Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu wanawake kupungua sekta ya kilimo

Dar es Salaam. Wakati kilimo kikichukuliwa kuwa sekta inayoajiri watu wengi nchini, hali ni tofauti miaka ya hivi karibuni, kwani takwimu zinaonyesha wamepungua kutoka wastani wa asilimia 74.5 mwaka 2004/05 hadi wastani wa asilimia 31 mwaka 2022.

Kwa mujibu wa ripoti ya idadi ya watu, Afya na Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS) ya mwaka 2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wanawake wanaofanya kazi katika kilimo wamepungua kwa kasi kutoka asilimia 78 mwaka 2004/2005 hadi asilimia 69 mwaka 2010, asilimia 56 mwaka 2015/2016 na asilimia 30 mwaka 2022.

"Asilimia ya wanaume wanaojihusisha na kilimo imepungua kutoka asilimia 71 mwaka 2004/05 hadi mwaka 62 mwaka 2010 na kutoka asilimia 59 mwaka 2015/16 na asilimia 32 mwaka 2022,” inasema ripoti hiyo. Pia, inaonyesha idadi ya wanaume wanaojihusisha na kazi za nguvu za ujuzi imepungua katika kipindi hicho.

Loading...

Loading...

Tofauti na matarajio ya wengi, ripoti hiyo inaonyesha idadi ya wanawake wanaojishughulisha na kilimo ni ndogo kuliko wanaume.

“Katika maeneo ya vijijini, watu wanne kati ya 10 wanajihusisha na kilimo, wanawake wakiwa asilimia 41 na wanaume asilimia 44, wakati kwa mijini ni asilimia 10 ya wanawake na asilimia 8 ya wanaume.” Ripoti hiyo inaendelea kuonyesha kuwa wanawake wenye umri kati ya 15–49 huajiriwa zaidi kwenye kilimo (asilimia 30) na kazi zisizo za ujuzi (asilimia 24), huku asilimia 32 ya wanaume wakiajiriwa katika kilimo.

Kuhusu ujira, ripoti inaonyesha kwa ujumla asilimia 50 ya wanawake walioajiriwa katika miezi 12 iliyopita, walilipwa fedha taslimu pekee na asilimia 14 walilipwa fedha taslimu na kwa bidhaa.

"Wanawake wanne kati ya 10 (asilimia 43) walikuwa wamejiajiri na asilimia 44 walikuwa wakifanya kazi kwa vipindi. Jinsi wanavyolipwa, wanayemfanyia kazi na jinsi wanavyofanya kazi mara kwa mara inategemea na kama wanafanya kazi katika sekta ya kilimo.

"Kwa ujumla nusu ya wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo hawalipwi. Wanawake wengi wanaojihusisha na kilimo ama wanawafanyia ndugu (asilimia 68) au wamejiajiri (asilimia 27).”

Ripoti pia inaonyesha wanawake wasio na elimu ndio wanaojishughulisha na kilimo (asilimia 46), ikilinganishwa na asilimia 14 ya walio na elimu ya sekondari au elimu ya juu.

Pia imeonekana kuwa wanaume wengi wasio na elimu wanajihusisha na kilimo (asilimia 48) ikilinganisha na asilimia 17 ya wenye elimu ya sekondari au elimu ya juu.

"Katika maeneo ya mijini huduma za mauzo zinaongoza kufanywa na wanawake (asilimia 31) na kazi za nguvu zinazofanywa na wanaume zinaongoza (asilimia 30).”


Kwa nini hali hiyo?

Mkurugenzi wa Malembo Farm na mdau wa Kilimo, Lucas Malembo alisema wakati mwingine ni ngumu kwa mtu kuendelea kulima, ikiwa hajapata tija ya kile alichokifanya kwa miaka miwili au mitatu mfululizo. Jambo hilo humfanya kuangalia njia nyingine inayoweza kumuingizia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yake.

“Lakini sekta ya kilimo Tanzania imeendelea kushuka kwa sababu kilimo kinashikiliwa na kundi la wazee, umri wa wakulima Mtanzania ni miaka 65, lakini Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonyesha kuwa vijana wako zaidi ya milioni 30, hivyo ni vyema kuweka mazingira mazuri kwa ajili yao na yanayotumia teknolojia za kisasa,” alisema.

Alisema ili kupiga hatua katika kilimo, pia ni vyema kuangalia namna ya kuongeza tija kwa kile alichoeleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa hekta moja nchini inaweza kuzalisha hadi tani 6, lakini kwa sasa wakulima wanaweza kuzalisha kati ya tani 1.9 hadi tani 1.7.

“Hili litafanikiwa pia kwa kutumia mbegu bora, kwa sasa wakulima wanaotumia mbegu bora ni asilima 28 pekee, tunapoongelea mbegu bora iwe ile inayofaa kwa uzalishaji, wengi wanadhani tunamaanisha mbegu zinazotengenezwa maabara,” alisema.

Alisema matumizi ya mbolea bora pia ni muhimu katika uzalishaji, ili kuwafanya wakulima waachane na kilimo cha mazoea kitakachowafanya washindwe kupata tija.

Ili kufanya watu wengi zaidi wajikite katika kilimo, Malembo alihamasisha matumizi ya teknolojia bora za kilimo za kisasa, ikiwemo matrekta katika kulima, kuwekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kama ilivyo azma ya Serikali.

Anachokisema Malembo kinafanana na Dk Festo Silungwe, mkuu wa idara ya uhandisi wa ujenzi na rasilimali maji kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kwamba huenda kukosekana kwa tija katika kilimo ikawa sababu ya watu kukacha kilimo. Pia, alisema kukua kwa matumizi ya teknolojia inaweza kuwa njia nyingine iliyopunguza nguvu kazi iliyokuwa ikitumika katika kilimo kutokana na kazi zao kufanywa na mashine moja. Akitolea mfano wa kilichotokea katika mashamba ya chai Kenya, alisema kukubali mashine zitumike katika kuvuna chai kulifanya watu zaidi ya 200,000 kupoteza kazi zao.

"Tunahitaji tafiti zaidi kujua watu walioondolewa na teknolojia ni wangapi, wameondolewa na masoko, ingawa sasa masoko ya bidhaa za kilimo yameongezeka,” alisema Dk Silungwe.

Alisema kinachotekea sasa ni picha inayoweza kuletwa na mabadiliko, huku akieleza kuwa linaloonekana ni sawa na kile kilichotokea katika nchi za Ulaya na Amerika miaka zaidi ya 100 iliyopita.

Alisema mabadiliko hayo hayataua sekta, bali itazidi kuimarika kwa sababu kampuni zinazouza matrekta zinaongezeka, jambo linaloashiria kuwa wanaolima kwa mikono wanapungua, mashine za kupanda mpunga zinaletwa na inarahisisha kazi.

"Mabadiliko ya teknolojia tuliyoyakumbatia yanatuleta katika sehemu nzuri ambayo wenzetu wameshapita miongo mitatu iliyopita,” alisema.

Maneno yao yanaungwa mkono na Lydia Alex, anayeeleza kukosa tija katika kilimo kama alivyokuwa akiambiwa na watu kulimfanya kutafuta shughuli nyingine ya kufanya.

"Nililima mara ya kwanza kiasi nilichowekeza hakikurudi, nikaangalia wapi nilikosea nikalima tena, nikawa nakaribia kufikia uwekezaji niliofanya, nilipolima mara ya tatu ukame unilitafuna na kila kitu kuharibikia shambani, nikaona bora niangalie kitu kingine,” alisema Lydia.