Mgambo adaiwa kujinyonga kisa ugomvi na mkewe

Muktasari:

  • Marehemu amedaiwa kutumia kamba ya manila kwenye kenchi chumbani chumbani kwake ambako hapakuwa na siling bodi kisha kupanda juu ya dumu na stuli na kujinyonga hadi kufa.

Kiteto. Shukurani Jackson (34) mkazi wa Kiegea, Kata ya Sunya, wilayani Kiteto, mkoani Manyara, amedai kujinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya manila chumbani kwake.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Sunya Kiteto wakiandaa mazishi ya Shukuru Jackson (34) askari mgambo aliyepoteza maisha kwa kujinyonga. Picha na Mohamed Hamad Kiteto

Marehemu amedaiwa kutumia kamba hiyo kwa kuifunga kwenye kenchi ya nyumba yake chumbani, ambako hapakuwa na dari kisha kupanda juu ya dumu na stuli na kutekeleza kitendo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP  George Katabazi, leo jumapili Novemba 12, 2023 amesema tukio hilo limetokea Novemba 11, 2023 Kiegea kata ya Sunya wilayani Kiteto.

“Marehemu alitumia kamba ya manila kuifunga chumbani kwake hapo hapakuwa na dari kisha kupanda juu ya dumu na stuli ili kuifikia na kujinyonga hadi kufa,” amesema ACP Katabazi.

Amesema marehemu hakuacha ujumbe wowote wa maandishi ingawa mwanzo alikuwa na ugomvi na mke wake ambaye walikuwa na watoto wawili, mmoja ana mwaka mmoja na nusu na mwingine miaka minne

“Marehemu alikuwa ana kawaida ya kulewa siku hiyo alitoka kazini yeye ni Askari mgambo huwa analinda shule ya msingi Sunya na alipofika nyumbani saa mbili alikorofishana na mke wake ambaye alikimbilia nyumbani kwao siku hiyo,” amesema Kamanda Katabazi.

Amesema baada ya kuona hivyo yeye alifunga nyumba na kurejea lindoni kwake hadi asubuhi ambapo alirejea nyumbani na kuchukua maamuzi hayo magumu.

"Alipofika nyumbani alikutana na mke wake asubuhi anaenda mtoni yeye aliingia ndani na kuchukua kamba ya manila na kujinyonga..mke aliporejea akakuta mume amefariki,"amesema Katabazi.

Naomba nitoe rai kwa wananchi waache kujinyonga kwani sio suluhu ya matatizo…ni vizuri mtu hata kama ana tatizo ashirikishe wenzake kabla ya kufanya uamuzi hayo ya kukatisha maisha yake kwani kwa kufanya hivyo sio suluhisho la matatizo yake.

“Nilipata taarifa kuwa marehemu alikutana na mke wake anaenda kwenye maji kisha kuingia ndani alichukua kamba ya manila na kujinyonga…mwanamke aliporejea nyumbani akamkuta mume wake amejinyonga ndani ndipo tukatoa taarifa Polisi,” amesema Musa Britoni Diwani kata ya Sunya.