Mke wa Askofu ajinyonga chanzo kikidaiwa maradhi ya saratani
Muktasari:
Mke wa Askofu Vitalis Sunzu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Biharamulo, Monica Vitalis (45) amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila jirani na Kambi ya hifadhi ya Burigi Chato kwa kile kinachodaiwa ni msongo wa mawazo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya tumbo muda mrefu.
Chato. Monica Vitalis (45), mkazi wa Kijiji cha Kasenga wilayani Chato Mkoa wa Geita ambaye ni mke wa Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Biharamulo, Vitalis Yusuph amekutwa amefariki kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila karibu na Hifadhi ya Taifa Burigi Chato.
Akitoa taarifa ya tukio hilo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake leo Ijumaa Novemba 10, 2023; Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema tukio hilo limetokea Novemba 8 mwaka huu katika kijiji cha Kasenga kata ya Kasenga wilayani Chato.
Kamanda Jongo amesema jeshi hilo lilipokea taarifa ya mwili wa mwanamke kuonekana ukning’inia juu ya mti na maofisa wa polisi walipofika eneo la tukio walibaini mwili huo ni wa mke wa Askofu aliyedaiwa kupotea.
“Ziliibuka tetesi kuwa mke wa askofu alipotea na kukutwa ameuawa, taarifa za awali zilionyesha amejinyonga lakini kwa hizo tetesi sisi polisi tulitaka kujiridhisha zaidi na tuliupeleka mwili Hospitali ya kanda ya Rufaa Chato na jopo la madaktari sita wameufanyia uchunguzi na kubaini alijinyonga,”amesema Jongo
Amesema kwa mujibu wa mume wake, mama huyo alikuwa akisumbuliwa na tumbo kwa muda mrefu hali iliyopelekea afanyiwe upasuaji mara mbili na hivi karibuni alikwenda hospitali na kubainika kuwa na maradhi ya Saratani.
Jongo amesema taarifa za kuugua Saratani zinadhaniwa kumpa msongo wa mawazo na kumfanya achukue maamuzi magumu ya kujinyonga.