Mganga wa kienyeji atupwa jela maisha kwa ubakaji

Mganga wa kienyeji, Kalebo Charles (46) akiwa chini ya ulinzi

Muktasari:


  • Amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kuchapwa viboko vitano baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne mkoani Kigoma

Kigoma. Mahakama ya Wilaya Kigoma, imemuhukumu kifungo cha maisha jela na kuchapwa viboko vitano, mganga wa kienyeji, Kebelo Charles (46), baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne.

Akisoma hukumu hiyo leo, Februari 28, 2024 Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Eva Mushi amesema mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri akiwemo daktari aliyempima mtoto huyo mwenye umri wa miaka 10.

Hakimu Mushi amesema mshtakiwa ametiwa hatiani chini ya kifungu cha 130(1) na (2) e na kifungu 131(1) cha kanuni ya adhabu namba 16 kama ilivyorekebishwa mwaka 2022 kifungo cha maisha na kuambatana na viboko vitano.

 “Ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapa kwa ujumla unaonyesha mwanafunzi huyo aliingiliwa sehemu zake za siri, jambo ambalo ni kielelezo tosha cha kosa la ubakaji na pamoja na umri wa mtoto huyo ambao ni miaka 10,” amesema Mushi.

Akieleza mwenendo wa shauri hilo wakati akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mushi amesema mshtakiwa awali alikuwa akiishi karibu na kufahamiana na familia ya mtoto huyo na alitenda kosa hilo Septemba 3, 2023, mchana alipokwenda nyumbani kwa familia ya mtoto huyo kusalimia.

Amesema baada ya kufika nyumbani kwa mtoto huyo alimkuta akicheza na mdogo wake mwenye umri wa miaka mitano, ndipo aliwachukua na kuondoka nao, huku akiwaambia anawapeleka kuwasalimia watoto wake.

Ameeleza kuwa mganga huyo aliwachukua na kuelekea nyumba ya kulala wageni iliyopo kata ya Mwanga Kaskazini, Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo watoto wake hawakuwepo kama alivyosema awali wakati wanatoka nyumbani.

Imeelezwa mganga huyo alitumia nafasi hiyo kumbaka mtoto huyo mbele ya mdogo wake akiona.

Baada ya tukio hilo, watoto hao walirudi nyumbani na kutoa taarifa kwa familia na ndipo mgang huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani na mashahidi saba wa upande wa Jamhuri walitoa ushahidi pamoja na vielelzo viwili.

Akizungumza baada ya kutolewa hukumu hiyo, Wakili wa upande wa Jamhuri,  Nestory Kuyula amesema haki imetendeka kwa mtoto huyo na kwamba hukumu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa  ya ukatili kwa watoto na wanawake.

Kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa madai ni yatima na ndiye mwenye jukumu la kulea wadogo zake.