Mgogoro wa kugombea mwili wa Mambya kumalizwa mahakamani
upande wa Mke mkubwa wakiwa wanaingia Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo. Picha na PraiseGod Mgumba
Muktasari:
- Wambura Mambya ambaye alikuwa mvuvi alifariki Julai 21, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure.
Mwanza. Mgogoro wa kugombania mazishi ya Wambura Mambya (54), umefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza huku pande zinazohusika zikianza kuonyesha dalili za kufikia mwafaka kuhusu namna ya kuendesha mazishi ya marehemu.
Shauri hilo namba 19355 la mwaka 2026, linalomhusisha Elizabeth Nyakao, anayedai kuwa ni mke mkubwa wa marehemu, dhidi ya John Mambya, limesikilizwa leo Jumanne, Julai 28, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Chrescencia Mushi.
Awali, kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa saa 5:00 asubuhi. Hata hivyo, wakati upande wa mwombaji ukiingia ndani ya chumba cha mahakama, baadhi ya ndugu wa marehemu walibaki nje wakieleza kuwa hawakufahamu utaratibu wa mahakama wala chumba sahihi cha kusikilizia shauri hilo.
Kutokana na kutokuwapo kwa upande wa ndugu wakati shauri lilipoitwa, mahakama iliahirisha kesi hiyo na kuipangia kusikilizwa Julai 30, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, Wakili Demetrius Mtete amesema migogoro ya aina hiyo mara nyingi hupata suluhu kupitia maridhiano ya pande husika badala ya hukumu ya mahakama.
Upande wa Ndugu wa Marehemu wakiwa wanaingia Mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo . Picha na PraiseGod Mgumba
"Kwa kawaida, kesi kama hizi zinahitaji makubaliano ya pande zote ili kufikia suluhu ya kudumu, kuweka usawa na kuepusha migogoro zaidi," amesema Mtete.
Hata hivyo, baada ya majadiliano, pande zote zimefikia makubaliano ya awali kwamba mwili wa marehemu utazikwa upande wa familia kwa kuzingatia mila na desturi zao.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwasilishwa rasmi mahakamani Julai 30, 2026 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Akizungumzia hatua hiyo, mke mkubwa, Elizabeth Nyakao amesema ameridhishwa na hatua ya makubaliano iliyofikiwa.
Wambura Mambya ambaye amekuwa akijishughulisha na shughuli za uvuvi, alifariki dunia Julai 21, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.