Mgombea CCM afariki muda mfupi kabla ya uchaguzi

Muktasari:

  • Aliyekuwa mgombea wa ujumbe wa mkutano mkuu Taifa na Halmashauri Kuu ya Wilaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Calisti Silayo amefariki dunia ghafla.

Rombo. Aliyekuwa mgombea wa ujumbe wa mkutano mkuu Taifa na Halmashauri Kuu ya Wilaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Calisti Silayo amefariki dunia ghafla.

Silayo amefikwa na mauti baada ya kujisikia vibaya muda mfupi kabla ya kuanza kwa uchaguzi uliofanyika ukumbi wa Shauritanga, leo Ijumaa, Septemba 30,2022.

Katibu wa CCM Wilaya ya Rombo, Mary Sule amesema, muda mfupi kabla ya uchaguzi kuanza kwa wagombea kujieleza, Silayo alijisikia vibaya na kupelekwa Hospitali Teule ya Huruma kwa matibabu.

"Alifika hapa kwenye uchaguzi, lakini kabla ya kuanza kwa uchaguzi alijisikia vibaya na akapelekwa Hospitali ambako alifariki dunia," amesema Sule

Diwani wa Katangara Mrere, Venance Maleli amesema kifo hicho kimemshtua kwani asubuhi ya leo aliingia ukumbini kwenye mkutano, lakini alisema anajisikia vibaya na ndipo taratibu zilifanyika kumpeleka hospitali Teule ya Huruma, lakini taarifa baadae zilirejea na kueleza amefariki dunia

Katika Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya tatu leo Ijumaa zimefanya uchaguzi wa CCM ngazi ya wilaya ambapo ni Moshi Vijijini, Same na Rombo na mpaka sasa taratibu za uhesabuji kura zinaendelea.