Prime
Mgombea udiwani naye adai kutekwa na wafuasi wa Baba Levo
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, akiwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma jana Juni 18, 2026.
Muktasari:
- Mbunge wa Kigoma Mjini, maarufu Baba Levo anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.
Kigoma. Shahidi wa 12 katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) Clayton Chipando, maarufu Baba Levo ameieleza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma matukio aliyoyaita ya ukiukwaji sheria za uchaguzi ikiwemo kutekwa kwake wakati wa uchaguzi huo.
Shahidi huyo Kacheche Kacheche, ambaye pia alikuwa mgombea udiwani, ametoa maelezo hayo katika ushahidi wake wa maandishi uliopokewa mahakamani na kuwa sehemu ya ushahidi wake katika kesi hiyo leo Jumatano Julai 9, 2026.
Baba Levo alitangazwa mbunge na Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne wanaojitambulisha kama wapiga kura jimbo la Kigoma Mjini, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela, Lumu Mwitu wamepinga ushindi wake na kuamua kufungua kesi.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 mbali na yeye Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji hao wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji sheria kanuni na taratibu za Uchaguzi, vikiwemo vitendo vya rushwa na udini vilivyofanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Katika maswali ya dodoso alipohojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola kuhusiana na maelezo ya ushahidi wake wa maandishi amesema amefika mahakamani kutoa ushahidi kuhusiana na vitendo vya kiharamia, utekaji na ukiukwaji wa sheria.
Alipoulizwa kama katika hati ya malalamiko kuna dai la uharamia amejibu kuwa hati hiyo hajaiona.
Kwa mujibu wa ushahidi wake huo shahidi huyo amedai yeye pia alitekwa Oktoba 29, 2026 huku akiwataja baadhi ya watu aliodai ndio walihusika na vitendo hivyo na kwamba watu hao ni wafuasi wa Baba Levo.
Pia ametaja baadhi ya watu anaodai walitekwa akiwemo Athumani ambaye ameeleza alitekwa na mgombea wa udiwani kata ya Kitoni Athuman Alphan, na kupelekwa kituo cha Polisi.
Alipoulizwa kama watu wanaotekwa huwa wanapelekwa polisi amejibu hajui na kama alipotekwa ndani ya gari alimowekwa alimkuta Baba Levo amejibu kuwa hapana.
Katika maelezo yake pia ameeleza mawakala wa chama chake walitolewa nje ya kituo na wakarudi baada ya saa mbili na alishuhudia tukio hilo lakini alipoulizwa kama amewataja majina yao mawakala hao katika maelezo yake amejibu hakuwataja.
Pia ameeleza aliomba fomu ya kusaini kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi lakini akanyimwa.
Hata hivyo, amejibu haijui fomu hiyo ni namba ngapi wala hajataja jina la msimamizi wa kituo hicho wala jina la kituo na kwamba hajawahi kufungua shauri.
Wakati akidodoswa na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, shahidi huyo amejibu katika maelezo yake hakuna mahali alipoeleza watu waliomteka walikuwa ni wafuasi wa Baba Levo, wala kwamba utekeji huo ulifanywa na Baba Levo.
Katika ufafanuzi wa majibu yake kutokana na maswali ya dodoso, akiongozwa na wakili wa walalamikaji, John Seka, amedai tukio alilofanyiwa ni utekaji kwa sababu alivamiwa akatupiwa kwenye gari na waliomvamia walifunika nyuso zao (walivaa mask), tofauti na ukamataji wa polisi.
Pia amefafanua kwenye gari alimkuta diwani aliyekuwa meneja wa kampeni wa Baba Levo na walikuwa wanasema Zitto hawezi kuwa mbunge wa jimbo hilo isipokuwa Baba Levo na wao ACT-Wazalendo walikuwa wanajidai wana watu lakini mbona wamemkamata kama kuku.
Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo imeiahirisha mpaka kesho, Ijumaa, Julai 10,2026, itakapoendelea kwa ushahidi wa mashahidi wengine.