Mgombea urais Kenya ashindwa kupiga kura

Mgombea urais wa tiketi ya chama cha Roots, George Wajackoyah

Muktasari:

  • Mgombea urais wa tiketi ya chama cha Roots, George Wajackoyah ameshindwa kupiga kura baada ya Teknolojia ya Uchaguzi ya Kielektroniki (Kiems) kushindwa kumtambua.

Nairobi. Mgombea urais wa tiketi ya chama cha Roots, George Wajackoyah ameshindwa kupiga kura baada ya Teknolojia ya Uchaguzi ya Kielektroniki (Kiems) kushindwa kumtambua.

Mgombea huyo mwenye sera za kipekee zikihusisha uzalishaji na uuzaji wa zao la bangi alifika kwenye kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi Indangalasia saa 4.15 kwa ajili ya kupiga kura huku maofisa wa kituo hicho wakisema kuwa mfumo wa kiems umesimama kufanya kazi ghafla hivyo wanasubiria maagizo kutoka ngazi za juu.

“Ungeanzia hapa. Lakini tunapitia changamoto. Tatizo liko kwenye mashine. Hakuna tunachoweza kufanya (sasa). Tumewasiliana na makao makuu, wakasema wanakuja. Iwapo itakuwa sawa, wapiga kura watapewa saa zao 11 kuanzia tutakapoanza,” afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) alimwambia Wajackoyah.

Wajackoyah ameonyesha kukubaliana na maelezo hayo na amesema ana Imani tatizo hilo litashughulikiwa kwa haraka.

“Ninashindwa kuelewa. Kwanini mfumo haufanyi kazi? Hamuwezi kupata nakala zenye utambulisho wetu na tukapiga kura? Lakini msijali. Hivi vitu hutokea ila kitu cha msingi tusisubiri siku Zaidi ya leo na tuna Imani changamoto hii itatatuliwa,”alisema Wajackoyah.