Mgombea wa CCM amrithi Lissu jimbo la Singida Mashariki

Muktasari:

  • Mgombea mbunge katika uchaguzi mdogo wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu amepita bila kupingwa baada ya wenzake 12 kushindwa kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo

Singida. Mgombea mbunge katika uchaguzi mdogo wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu amepita bila kupingwa baada ya wenzake 12 kushindwa kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo.

Mtaturu ametangazwa leo Ijumaa Julai 19, 2019 saa 10 jioni na ofisa uchaguzi Wilaya ya Ikungi, Jonal Katanga baada ya kutowekewa pingamizi lolote.

Mtaturu amekabidhiwa cheti cha ubunge wa jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na Tundu Lissu tangu mwaka 2010 hadi Juni 28, 2019.

Mbunge huyo mteule alirejesha fomu jana kabla ya saa 10:00 jioni, muda ambao wagombea wote waliochukua fomu walitakiwa kuwa wamezirejesha.

Wagombea wengine waliochukua fomu ni Hamidu Hussein (ADA-Thadea), Tirubya Mwanga (UPDP), Ameni Npondia (CCK), Amina Ramadhan (DP), Ayuni John (UDP), Amina Mcheka (AAF), Maulid Mustafa (ADC), Selemani Ntandu (CUF), Feruzy Fenezyson (NRA), Abdallah Tumbo (UMD), Donald Mwanga (TLP) na Masalio Kyara (SAU).

Uchaguzi katika jimbo hilo umepangwa kufanyika Julai 31, 2019  kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Lissu aliyepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni na utoro bungeni.

Fomu ya Mtaturu ilibandikwa katika ubao wa matangazo wa ofisi ya halmashauri ya Ikungi ili kutoa fursa ya watoa pingamizi hadi leo saa 10 jioni.

Lissu yupo nje Tanzania tangu Septemba 7, 2017 akitibu majeraha ya risasi alizomiminiwa akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea.