Mgomo wa madaktari Kenya wakimbilia nchini

Rombo/Arusha. Wagonjwa raia wa nchini Kenya wameanza kuingia Tanzania kutafuta huduma za matibabu kutokana na mgomo wa madaktari na maofisa tabibu wa hospitali za umma nchini humo unaoendelea, huku idadi ya wagonjwa ikiendelea kuongezeka.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini uwepo wa ongezeko la wagonjwa kutoka Kenya katika hospitali zilizopo jirani na mpaka wa Kenya na Tanzania katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro na Longido, Mkoa wa Arusha.

Wakati hali katika hospitali za wilaya hizo mbili ikiwa hivyo, uongozi wa Serikali mkoani Mara umekaa mguu sawa kufuatilia wagonjwa watakaovuka mpaka na kuingia kutoka Kenya kwa lengo la kutafuta huduma ya matibabu.

Mgomo wa madaktari wa hospitali za umma Kenya ulianza Machi 15, mwaka huu ukihusisha wanachama wa Umoja wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU), unaotajwa kuwa na wanachama karibu 7,000 nchini humo.

Miongoni mwa madai ya madaktari hao ni kushinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao, kuajiriwa kwa mkataba kwa madaktari wanafunzi, kukatiwa bima ya matibabu kwao na wategemezi wao na kuchelewa kulipwa mshahara.

Mbali na madaktari hao, mgomo huo ulioingia wiki ya tatu sasa umeongezewa nguvu na maofisa tabibu ambao wamejiunga na kuvuruga huduma za matibabu katika hospitali za umma nchini humo.

Huo ni mgomo wa pili baada ya ule wa mwaka 2016/17 kudumu kwa siku 100 ukienda sambamba na mgomo wa wauguzi 45,000 nchi nzima na maofisa tabibu uliodumu kwa siku 20. Kama ilivyo baadhi ya raia wa Kenya kuingia nchini kutokana na mgomo huo, mwaka 2017 Wakenya waliingia nchini, akiwamo Bahati Tabu (37), aliyejifungua pacha watano katika Hospitali ya Faraja, wilayani Himo Mkoa wa  Kilimanjaro.

Mgomo huo uliohusisha madaktari na wauguzi zaidi 5,000 wa hospitali za Serikali ulianza Desemba 6, 2016, huku zaidi ya wagonjwa 40 wakipoteza maisha, hivyo Bahati aliamua kukimbilia Tanzania ili kujifungua.


Hali ilivyo sasa Kilimanjaro

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi baada ya kufika katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma pamoja na Hospitali ya Ngoyoni wilayani Rombo, umebaini uwepo wa baadhi ya wagonjwa waliotoka Kenya kupatiwa huduma maeneo hayo.

Baadhi ya wagonjwa waliokuwepo hospitalini hapo ambao wametokea Loitokitok Kenya, walisema wameamua kufuata huduma hiyo Tanzania, kutokana na mgomo unaoendelea nchini kwao.

Mmoja wa wazazi aliyemfikisha mwanaye hospitalini hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema alitumia usafiri wa bodaboda akitokea nchini humo, ili kunusuru maisha ya mwanaye kwa sababu huduma za hospitali binafsi Kenya ni ghali.

“Tumekuja hapa kwa sababu nchini kwetu kuna mgomo wa madaktari na kwa sababu sisi na Tanzania ni majirani, tukaamua kukimbilia huku kunusuru maisha ya ndugu zetu, ni umbali mrefu. Nimetumia zaidi ya Sh15,000 kwa bodaboda hadi kufika hapa,” alisema mama huyo na kuongeza;

“Licha ya gharama kubwa za usafiri hadi kufika hapa, mtoto wangu amepewa huduma ya kwanza, lakini kutokana na hali yake kutokuwa nzuri, tumepewa rufaa kwenda Hospitali ya KCMC kwa matibabu makubwa zaidi.”

Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema wagonjwa kutoka nchi jirani wapo, lakini idadi yao si kubwa kama ilivyotokea kwenye mgomo wa Desemba 2016 hadi 2017.

“Wagonjwa wapo, lakini si wengi sana kama kipindi kilichopita, kipindi kile wagonjwa walifurika na wengine waliletwa hadi na mabasi kuja kutibiwa hapa, hali iliyosababisha tufanye kazi usiku na mchana,” alisema.

Akizungumzia ongezeko la wagonjwa kutoka Kenya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Deogratius Maruba alisema baadhi ya hospitali za wilaya hiyo wameongezeka, tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya mgomo huo.

"Kwenye baadhi ya vituo kumekuwa na ongezeko la wagonjwa kutoka Kenya mara mbili ya waliokuwepo, hasa katika Hospitali ya Ngoyoni," amesema mganga huyo.

Akizungumzia hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jairy Khanga alikiri kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma vya mpakani, hususan Rombo, huku akisema ongezeko zaidi ni la wajawazito na watoto.

“Ni kweli kuna ongezeko kubwa, na hii taarifa nimeipata Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, wajawazito wengi na watoto wamekuja kupata huduma kwenye hospitali na vituo vyetu, lakini hili ongezeko halijaathiri utoaji wa huduma huku kwetu,” alisema Khanga.

“Serikali haiwezi kujipanga kwa issue ya Kenya, lakini tumeliona hili, kuongezeka kwa wagonjwa kutoka kwa jirani zetu Kenya na mkakati ambao tunataka tuende nao sasa ni lazima hawa wenzetu wachangie huduma za afya ambazo huku hatuchangii.

“Bila hivyo, rasilimali zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya watu wetu hazitatosha. Gharama ambazo hazitozwi kwa Watanzania, ikiwamo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, kwa hawa wenzetu tutawatoza.

“Lakini tunataka kushirikiana na watu wa uhamiaji, ili kuona kwamba hao watu wanapokuja kupata huduma wamepitia kwenye njia sahihi za kuingia nchini," alisema Khanga.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi upande wa Horohoro mkoani Tanga, umebaini kuwa hakuna dalili za wagonjwa kuingia.


Hali ilivyo Longido

Kama ilivyo Rombo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Wilaya ya Longido, Dk Mathew Majani naye alisema kwa sasa katika Kituo cha afya Orendeke hali ya wagonjwa wanaotoka Kenya imeongezeka.

Eneo la Namanga wilayani Longido ni mpaka kati ya Tanzania na Kenya, Dk Majani alisema licha ya kutokuwa na takwimu sahihi, idadi ya wagonjwa kutoka nchini humo imeongezeka tangu kuanza kwa mgomo huo Machi, mwaka huu.

“Ikizingatiwa hapa ni eneo la mpakani, kwa taarifa nilizonazo zinaonyesha idadi ya wagonjwa wanaotoka Kenya kuja kupata huduma za kiafya, hasa Kituo cha Orendeke imeongezeka, tofauti na ilivyokuwa awali," alisema Dk Majani.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marko Ng'umbi alisema  kwa asili watu wa eneo hilo ambao ni raia wa Kenya na Tanzani huingiliana.

Alisema raia wa Kenya hufika kupata huduma upande wa Tanzania, halikadhalika Watanzania huingia Kenya kupata huduma, zikiwamo za afya na masoko.

“Kiukweli baada ya mgomo wa madaktari na wauguzi nchini Kenya, bado hatujaangalia kama kumekuwa na ongezeko zaidi la wagonjwa, nadhani kwa sasa tutaanza kufuatilia na kuliangalia hilo,” alisema.

Wakati madaktari na wauguzi wakigoma kutoa huduma kwa wagonjwa wakishinikiza kuboreshewa masilahi yao, uongozi wa Mara umekaa mguu sawa kufuatilia wagonjwa watakaovuka mpaka kuingia mkoani humo kwa lengo la kupatiwa matibabu.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Tarime Vijijini, Joseph Mziba alisema tayari wasimamizi wa vituo vya afya vilivyopo mpakani wilayani humo wameshapewa mwongozo wa hatua za kuchukua kubaini mgonjwa aliyeingia kutoka Kenya.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Janeth Joseph na Florah Temba (Rombo), Janeth Mushi (Arusha) na Mgongo Kaitira (Mwanza).