Mhagama: Kampuni 500 za vijana zipo wapi? zinafanya nini?

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ripoti ya usambazaji na uchambuzi wa Sera ya Biashara ya vijana jijini Dodoma. Picha na Mpiga picha wetu

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikihimiza vijana kujiajiri na kufanya biashara ili kupambana na ukosefu wa soko la ajira nchini, Wadau wameeleza changamoto zinazowakumba kuanzisha biashara hizo ikiwemo masharti magumu yasiyotekelezeka kwenye uchukuaji wa mikopo benki.

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amehoji zilipo Kampuni mpya zaidi ya 500 za vijana zilizosajiliwa nchini na kuagiza zifuatiliwe kujua hatma zake.

Mhagama amewaagiza Makatibu wakuu kuzifuatilia kampuni hizo kujua ziko wapi, zinafanya nini na nani anazifuatilia.

Waziri Mhagama ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Oktoba 19, 2023 wakati akizungumza baada ya kupokea wasilisho la ripoti na uchambuzi wa sera ya biashara ya vijana iliyofanywa kwenye mradi wa ‘Feed The Future’ ili kuondoa urasimu na kuwaimarisha vijana kujua mbinu za kufanya biashara na kujiajiri hususan kwenye sekta ya kilimo.

“Huko nyuma niliwahi kuhudumu kama waziri mwenye dhamana ya vijana na Makatibu wakuu mpo hapa nataka kuwapa hiyo kazi, kuna kipindi tulisajili kampuni mpya za vijana zaidi ya 500, lazima tuulizane hapa zipo wapi, zinafanya nini na nani anazifuatilia?

“Tumeona tunazungumzia hizo sera nzuri ambazo tunazitaka, sasa hizo kampuni tuziunganishaje kwa kuanza kuzifanya kutumia mazingira ya sera zilizopo kwasasa ili kuhakikisha zinakuwa ni sehemu ya mageuzi makubwa ya uchumi hapo baadaye,"amesema Mhagama.

Aidha Mhagama amesema Serikali itashirikiana kwa pamoja na wadau kutafuta suluhu ya changamoto zilizobainika kwenye ripoti hiyo na kuyafanyia kazi ili kuondoa vikwazo na kufanya mazingira ya kujiajiri, ufanyaji biashara na ujasiriamali kuwa mepesi na yatakayomhamasisha kila kijana aweze kuiona njia kwenye sekta binafsi.


Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilieleza kuwa hadi kufikia mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na upungufu wa ajira kwa asilimia 8.9 ambao ni changamoto kwa vijana ambao asilimia 56 kati yao ikiwa ni vijana wenye umri kati ya 15 na 35.

Awali akitoa wasilisho la ripoti hiyo Mshauri Mkuu wa mradi Dk Onesmo Shuma amesema ripoti hiyo imeonsha changamoto za uwepo wa sera mbalimbali zilizopitwa na wakati ambazo nyingi zina urasimu katika uanzishaji wa biashara kwenye sekta binafsi kwa vijana.

“Sera za sasa hazichukui mienendo ya kimataifa na miundo ya biashara inayohusiana na maendeleo ya biashara ya vijana, Ingawa huenda vijana hawajui manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na sera hizi kwenye biashara zao, vijana wengi wanahisi wameathiriwa vibaya na kutotekelezwa kwa usawa na utekelezaji wa dharura wa sera hizi”amesema.

Changamoto nyingine ukosefu wa huduma za kifedha licha ya kuwepo kwa programu za mikopo za vijana zinazoongozwa na serikali huku benki binafsi zikilalamikiwa kuwa na masharti yasiyotekelezeka kwa vijana wanaoanza biashara au kujiajiri.

Dk Shuma amesema changamoto nyingine ni ufikiaji mdogo wa vijana kwenye ardhi, soko, miundombinu, ukosefu wa huduma za usaidizi na kuanzisha mfumo wa ikolojia na mabadiliko ya hali ya hewa hususan kwenye sekta ya kilimo.

Justin Nkundya, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam amesema changamoto kubwa kwa vijana kujiajiri ni kukosa kuaminika katika taasisi za kifedha pale wanapoenda kuomba mikopo.