RC Shigella akerwa kipato duni cha wananchi Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Maartine Shigella
Muktasari:
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Geita una watu zaidi ya milioni 2.9, sawa na ongezeko la asilimia 5.4 la watu zaidi ya milioni 1.7 milioni kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewataka viongozi na wataalam mkoani humo kukuna vichwa kubuni na kutekeleza mikakati itakayoongeza pato la mwananchi mmoja mmoja mkoani humo kutoka wastani wa dola 1 ya Kimarekani, sawa na zaidi ya Sh2, 300.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi wa makundi mbalimbali mkoani Geita, Shigela amesema pato la wananchi hauakisi kiwango cha asilimia 7 ya mchango wa mkoa huo kwenye pato la Taifa.
Pamoja na utajiri wa madini ya dhahabu unaoufanya Mkoa wa Geita kutoa zaidi ya asilimia 40 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini, mkoa huo pia umejaaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Ukiacha uchumbaji madini na kilimo cha kutegemea mvua na cha umwagiliaji kutokana na baadhi ya maeneo ya mkoa huo kupakana na Ziwa Victoria, shughuli nyingine za kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Geita ni ufugaji, biashara na huduma.
Kutokana na wingi wa rasilimali, Shigela amewataka viongozi na watendaji kila mmoja kwa nafasi na eneo lake kufanya linalowezekana kuongeza pato na mwananchi mmoja mmoja unaoakisi mchango wa mkoa huo kwenye pato la Taifa.
“Wakati pato la wananchi wa Geita ni sawa na dola moja kwa siku, sawa na takriban Sh2, 300, wenzetu wa Dar es Salaam kipato cha mtu mmoja mmoja ni Sh5, 000 huku kwa Mkoa wa Mbeya ni Sh4, 000,’’ amesema Shigella
Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) amewahimiza kila mwenye dhamana ya uongozi mkoani Geita kufanya jitihada zitakazoongeza ustawi katika sekta ya biashara, uzalishaji mali na uwekezaji na hatimaye pato la mtu mmoja mmoja.
Amesema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni miongoni mwa nyezno muhimu zinazotakiwa kutumika kutunga sera, kupanga, kutekeleza na kufuatilia mipango ya maendeleo kukuza uchumi na ustawi wa watu na Taifa kwa ujumla.
Meneja wa Takwimu Mkoa wa Geita, Khalid Msabaha amesema mkoa huo una zaidi ya watu milioni 2.9 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 5.4 la watu zaidi ya milioni 1.7 milioni waliohesabiwa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 55.7 ya wakazi wa mkoa huo ni watoto wenye umri chini ya miaka 18 wakati idadi ya vijana ni asilimia 33.5 huku wazee wakiwa asilimia 3.9.
Katika idadi hiyo, zaidi ya watu milioni 1.03 wanaishi Halmashauri ya Geita wakati watu 584, 963 wako Halmashauri ya Wilaya ya Chato huku Halmashauri ya Wilaya ya Nyangwale yenye idadi ndogo zaidi ikiwa na watu 225,803.
Halmashauri ya Mji Geita ina watu 361,671 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ina watu 211,747 huku Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ikiwa na watu 396,423. Mkoa wa Geita ina halmashauri sita zilizoko ndani ya wilaya zake tano.