Miaka 32 ya chukizo hadi wito kwenye ualimu

mwalimu Wande Nkonyi akiwa na wanafunzi wake darasani

Alianza kama mwalimu wa daraja la tatu A, akajiendeleza sasa ni msomi wa shahada na Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi Tuangoma iliyopo Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Akisimulia safari ya maisha yake, anasema haikuwa rahisi kwake kufika hapo kwa sababu awali ualimu haukuwa kwenye ndoto zake.

Moyoni alitamani kuwa mwanajeshi au kusomea ufundi wa magari, ndio maana alipomaliza masomo ya sekondari na kupangiwa ualimu, alijitahidi kuukimbia.

Hata hivyo, majaliwa ya Mola hayakuwa upande wake, akalazimika kuusoma ualimu kwa shingo upande ili tu airidhishe familia.

Huyu ni mwalimu Wande Nkonyi ambaye licha ya awali kutoukubali ualimu, baadaye alipoingia kikamilifu kwenye fani, akajikuta akibadili fikra na kufuta kabisa ndoto alizokuwa nazo awali.

Ualimu ukatoka kuwa chukizo hadi kuwa wito kwake. Ndio maana haikuwa tabu kwake kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu, kibarua kinachowakimbiza walimu wengi shuleni.


Simulizi alivyosomea ualimu

Akieleza safari ya kuwa mwalimu, mwalimu huyo aliyeanza kufundisha mwaka 1991 anasema:

‘’Kiukweli sikuwahi kuwaza kuwa nitakuja kuwa mwalimu, lakini nilipopata nafasi ya kujiunga na chuo cha ualimu Monduli, Arusha kama mwalimu wa daraja la tatu A yaani wa shule ya msingi na namna nilivyokuwa nikiwasikia watu wa karibu wakiuzungumzia vibaya ualimu, nilijikuta ninatoka Arusha kuja Dar es Salaam kujificha ili nisiende kusoma katika chuo hicho nilichopangiwa.’’

Anasema kuwa kipindi kile wanafunzi waliokuwa wanasomea ualimu, walikuwa wakifuatiliwa sana, hivyo ilitumwa telegramu kwa wazazi wake kutoka chuoni ujumbe ukihitaji watoe maelezo kwa nini hakuwa amefika chuoni.

‘’Baada ya baba kumfahamisha mjomba wangu aliyekuwa Dar es Salaam juu ya ujumbe walioupata kutoka chuoni, alikasirika sana kwa nini sikuieleza familia kuwa nilipata nafasi ya kwenda chuo, hivyo ilinilazimu kurudi tena Arusha kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuelekea chuoni Monduli.

Bahati mbaya nilipofika Arusha nilikuta baba amesafiri kwenda Nairobi, hivyo ilinilazimu kumsubiri kwa takribani mwezi mmoja hadi aliporudi ndipo nikaanza maandalizi ya kwenda chuoni,’’ anasema na kuongeza:

Kipindi ninaripoti chuoni zilikuwa zimebaki siku chache kuanza kwa mitihani ya kumaliza muhula wa kwanza.

Hivyo niliuliza wenzangu masomo ya msingi ya ualimu na kile walichojifunza, nilitumia siku chache hizo kusoma na ilipofika siku ya Jumatatu niliingia na kufanya mitihani na Mungu ni mwema masomo yote ya msingi nilifaulu kwa alama B hivyo kuniruhusu kuendelea na masomo yangu ya ualimu.’’


Siku za mwanzo kazini



‘’Kwa kipindi cha mwanzo naanza kazi hii ni kweli nilijuta sana maana mshahara wangu kwa kipindi hicho ulikuwa Sh5,200 ambao ulikuwa hautoshelezi mahitaji, yaani nikinunua vyakula tu pesa imeisha.Nilikuwa nashindwa kununua hata nguo ambazo zitaongeza umaridadi wangu ninapokuwa kazini.

Nakumbuka nilitamani kushona suruali ambayo gharama yake niliambiwa na fundi ni Sh6,000 huku mshahara ni Sh 5,200.Hivyo ilinilazimu kuilipa Sh 6000 hiyo ndani ya miezi mitatu ndio nikaweza kuipata suruali.

Lakini, kadri siku zilivyokuwa zinazidi kwenda, nikajikuta pamoja na changamoto zote nazopitia nazidi kuifurahia na kuipenda kazi yangu kiasi cha kushawishi mtoto wangu naye kusomea ualimu.’’


Alichojifunza miaka 30 ya ualimu

Anasema kwa miaka yote 32 aliyotumikia fani ya ualimu, amejifunza kuwa ualimu ni wito kwani kupitia mwalimu unaweza kujenga au kubomoa wanafunzi, unaweza kutengeneza watoto wenye uthubutu katika yale yaliyo mema au kinyume chake.

‘’Nakumbuka kipindi ninaanza kuwa mkuu wa shule hii wanafunzi wengi walikuwa waoga kugombea nafasi za uongozi, niliwahamasisha na walipata uthubutu wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi walipofika ngazi ya sekondari.

Pia nimejifunza ualimu unahitaji ujifunze mambo mapya kila siku na unakuhitaji kuendana na wakati uliopo. Mfano, wakati huu mambo yanakwenda kidijitali, hivyo ni lazima kwa mwalimu kuhakikisha anajifunza vyema masuala yahusuyo Tehama ili kuendana na wakati tuliopo sasa.

Ukiwa mwalimu ni lazima uwe na moyo wa kujitolea kuisaidia jamii inayokuzunguka ikiwemo wanafunzi unaowafundisha, wajane, watoto yatima pale ambapo wanapata changamoto fulani za kimaisha.

Kwa mfano mimi binafsi nimeweka program ya kusaidia watoto kama 10 wenye mahitaji mbalimbali kama fedha ya chakula, nauli pamoja na mahitaji mengine. Hivyo unapokuwa mwalimu unatakiwa kujitoa kwa hali na mali kwa jamii.’’


Changamoto kazini

Kama walivyo walimu wengine, naye Analia na mtazamo potofu walionao watu wengi kuhusu kada hiyo ya utaalamu.

Anasema walimu hawathaminiwi, kwa wengi walimu ni watu duni ndio maana hata mwalimu anapojitutumua na kununua mfano gari, wapo watu wanaofikia hatua ya kuhoji uwezo huo.

‘’Unakuta mwalimu akifanikiwa kununua gari, baadhi ya wanajamii hushangaa na kuhoji amelipata vipi. Kutokana na maisha ya baadhi ya walimu kuwa duni, hujikuta wakiingia katika mikopo ambayo wengine hushindwa kulipa,’’anaeleza.

Anagusia ukosefu wa motisha kwa walimu hasa wanaofundisha katika maeneo yenye mazingira magumu…’’ hawa wanahitaji motisha ambazo zitaonyesha kile wanachokifanya kinathaminiwa na kinaonekana.


Anachokikumbuka ndani ya miaka 32

‘’Matukio mazuri katika ualimu ambayo nayakumbuka ni pamoja na kupata nafasi ya kwenda kusoma Malawi mwaka 1994. Nilikwenda kusoma elimu maalum kwa muda wa miezi mitatu.

Pia mwaka 2000 nilichaguliwa kuwa msimamizi wa programu ya Mobile Teaching kwa mkoa wa Dar es Salaa na 2017 kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa nidhamu kwa walimu wa msingi na sekondari wa Manispaa ya Temeke,’’ anasema.


Walimu wa sasa VS wa zamani

Akielezea tofauti kati ya walimu wa sasa na wa zamani, mwalimu huyo baba wa watoto anasema walimu wa sasa wanakabiliwa na utovu wa nidhamu hivyo kusababisha kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Anatoa mfano wa namna baadhi yao wanavyochelewa kufika kazini, matumizi ya lugha isiyo na staha kwa wanafunzi, walimu wenzao na hata wazazi. Anasema wengi wanashindwa kuzingatia miiko ya ualimu.

Kuhusu hadhi ya walimu, anasema: ‘’Hadhi ya ualimu bado inafunikwa na mitazamo ya kizamani. Unachukuliwa kama ni kazi inayofanywa na watu waliokosa kazi nyingine za kufanya, hivyo nashauri Serikali iangalie namna ya kuzidi kuboresha hadhi ya watu hawa muhimu katika jamii kwa kufanya yafuatayo;

Mosi, vyuoni iwe moja kati ya kozi ya vipaumbele ikiwezekana watakaochaguliwa kusoma ualimu wawe na ufaulu wa juu yaani daraja la kwanza na la pili pekee.

Pili, masilahi yao ikiwemo mshahara yaboreshwe zaidi kutokana na kazi muhimu wanayofanya katika jamii pamoja na kupewa kipaumbele katika teuzi za nafasi mbambali serikalini.


Anachofanya nje ya ualimu

Mimi ni mbunifu huwa muda wangu wa ziada huwa ninautumia kubuni zana za kufundishia na hadi sasa nilizobuni zinaweza kutumika kwa ngazi ya elimu ya awali. Zana hizo ni pamoja na T learning, kujifunza kwa kutumia kifurushi cha namba, pamoja na dawati safisha naosha Pamoja na hilo pia ninajishughulisha na udalali, ufugaji na kilimo. Pia nimewahi kuhudumu kama mwenyekiti wa serikali ya mtaa kwa takribani miaka 10.