Mifumo yaongeza ukusanyaji mapato Zanzibar

Muktasari:

  • Naibu wa waziri Fedha na Mipango, Ali Suleiman Mrembo amesema ukusanyaji mapato visiwani humo umeongezeka kwa asilimia 67 na hii ni kutokana na mifumo waliyoweka kuthibiti upotevu wa mapato hayo.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema uwapo na udhibiti wa matumizi ya mifumo umesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 63 kwa kipindi cha miezi tisa.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 10, 2023 na Naibu wa waziri Fedha na Mipango, Ali Suleiman Mrembo wakati akijibu swali la mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar ambaye alitaka kujua mkakati wa serikali kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.

Akijibu swali hilo, Naibu waziri amesema hakuna upotevu wa fedha zinazokusanywa badala yake imeongeza makusanyo hayo ambapo kwa kipindi cha miezi tisa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imekusanya Sh449.2 bilioni ya makadirio ya kukusanya Sh460.4 bilioni.

"Makusanyo haya ni ongezeko la Sh274.7 bilioni sawa na ukuaji wa asilimia 63.5 ya kipindi cha miezi 9 kwa mwaka 2021/23," amesema 

Amesema kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), makusanyo ymaeongezeka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2021/22 huku mapato yasiyo ya kodi yamefikia Sh67.2 bilioni.

Amesema Serikali katika udhibiti zaidi wa upotevu wa mapato ni pamoja na kuanzishwa na kuimarisha Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani za Serikali, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, CAG, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA).

Pia uanzishwaji wa mifumo kama BAMAS, Zan-Malipo, VFMS, ZIDRAS na kuwajengea uwezo watendaji huku akihitimisha kwa kusema hatua hizi zinathibitisha kuwa Serikali inaendelea kudhibiti upotevu wa mapato.