Migogoro 45 ya kifamilia huripotiwa kila mwezi Bukoba

Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Bukoba, Japheti Kanoni

Muktasari:

Migogoro ya familia 45 hupokelewa kila mwezi katika Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Bukoba. Migogoro ya familia 45 hupokelewa kila mwezi katika Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Bukoba, Japheti Kanoni amesema baadhi ya migogoro hiyo inahusisha vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake leo Jumanne Desemba 5, 2023, Kanoni ametaja migogoro ya familia na unywaji wa pombe kupita kiasa kuwa miongoni mwa sababu za migogoro inayoripotiwa kila mara ofisini kwake.

Akitaja takwimu, Ofisa Ustawi huyo amesema kati ya April hadi Septemba, 2023, ofisi yake ilipokea taarifa ya matukio manne ya ukatili wa kudhuru mwili, matukio matatu ya ukatili wa kingono, matukio 48 ya ukatili wa kihisia 48 na matukio mengine 20 ya ukatilia wa kutelekeza familia.

Judith Mwakyusa, wakili wa Serikali mwandamizi Mkoa wa Kagera ansema jumla ya kesi 68 za vitendo vya ukatili wa kijinsia ziliripotiwa na kufikishwa mahakamani kati ya mwezi Agosti hadi Novemba, 2023 ambapo kati ya hizo, Jamhuri ilishinda kesi 48 na washtakiwa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

‘’Jamhuri inashindwa au kulazimika kuondoa baadhi ya kesi mahakamani kwa kukosa ushahidi kwa ama walalamikaji kutohudhuria au wengine kuelewana na kumalizana na watuhumiwa mitaani,’’ amesema Judith

Bila kutaja jina, wakili huyo ametoa mfano wa kesi ya binti aliyebakwa na kupewa ujauzito ambaye awali alikiri kumfahamu mtuhumiwa na kuwa tayari kutoa ushahidi, lakini akageuka baadaye.

Amesema Wilaya ya Bukoba ndiyo inayoongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa na matukio 16, ikifuatiwa na Wilaya ya Missenyi yenye matukio 15, Muleba ikiwa na matukio 14, Wilaya ya Biharamulo ikiwa na matukio 10, Wilaya ya Ngara manane, Kyerwa matukio matatu na Wilaya ya Karagwe ikiwa na matukio mawili.